NA ZAINAB ATUPAE

TIMU ya Tupogo imefanikiwa kubeba ubingwa wa mashindano ya Bwejuu Super Ndondo Cup, baada ya kuichapa kwa penalti 4-2 dhidi ya Kazi Kazi, katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo.

Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa BZL Bwejuu majira ya saa 10:00 jioni,ulikuwa na mashabiki wengi wakiwemo wanaume na wanawake.

Katika mchezo huo hadi dakika 90 zinamalizika wanaume hao walitoka sare ya kufungana bao 1-1, ndipo sheria ya mikwaju ya penlati ilipotumika ili kutafuta bingwa.

Tupogo ndio iliyoanza kupata bao ambalo lilifungwa na Hassan Ameir dakika ya 31,huku dakika ya 61 Abdisara Ayoub wa timu ya Kazi Kazi alisawazisha bao.

Mabingwa hao walipata dume la Ng’ombe lenye thamani ya milioni 1.5, na mshindi wa pili Kazi Kazi ilijichukulia Mbuzi wawili wenye thamani ya shilingi 700,000.

Zawadi nyengine zilikwenda kwa wachezaji bora,timu bora,waamuzi bora na kipa bora.

Katika fainali hiyo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Halmashauri Wilaya ya Kusini Unguja Kassim Mtoro Abuu.