KWA kawaida uchaguzi wa kidemokrasia ni mchakato unaopitia kwenye hatua mbalimbali kabla ya kuifikia siku ya mwisho nayo ni kutangazwa kwa washindi waliogombea nafasi mbalimbali za kisiasa walizoomba.

Miongoni mwa hatua muhimu kwenye uchaguzi ni pamoja na kuandikishwa wapiga kura, uteuzi wa wagombea, kampeni, zoezi la upigaji kura, zoezi la kuhesabu kura na zoezi la kutangaza washindi.

Hatua za kwenye mchakato wa uchaguzi ni kama mnyororo baada ya kutoka hatua moja unakwenda hatua nyengine na kwamba huwezi kuiepuka ngazi moja kwa kufikiri kuwa sio muhimu na kuchupia nyengine.

Kuiepuka hatua moja kwa kudhani kuwa sio muhimu ni kuutia kasoro kiasi cha kuliharibu zoezi zima uchaguzi.

Tuipongeze sana Tume ya Uchanguzi Zanzibar (ZEC), kwa jinsi inavyosimamia uchaguzi wa mwaka huu hatua kw ahatua, hivi sasa tukiwa kwenye kampeni na hakuna hatua iliyokiukwa.

Hata hivyo, katika kipindi hichi cha kampeni ambapo wagombea kutoka vyama mbalimbali vya siasa wakiwa na fursa ya kueleza sera na ilani zao wakati mwengine fursa hiyo hutumiwa vibaya.

Maana ya kampeni kwa muktadha wa siasa za Zanzibar ni fursa ya wagombea kupita kwa wananchi kuwaomba, kuwabembeleza ili wawachague na kuwaeleza nini utawafanyia endapo watakuchagua.

Kwa masikitiko makubwa baadhi ya vyama vya siasa hawaitumii vyema fursa ya kampeni kueleza ilani na sera zao, badala yake vinaonekana vina ashiria kuhamasisha na kupandikiza chuki na mifarakano katika jamii.

Kwa mfano bado wapo wanasiasa kwenye mikutano yao ya kampeni zinazoendelea wanahamasisha wananchi hasa vijana kuandamana pasi na kuzingatia misingi ya sheria.

Ni vyema tuwaeleze wananchi na kwa hili watuelewe kwamba maandamano yanayohamaishwa na wanasiasa kama yatakosa kuafuata misingi ya sheria ikiwemo yatakuwa kinyume cha sheria.

Maandamo sio haramu hapa nchini kwetu, lakini kitu cha muhimu yazingatie sheria na wasimamizi wajiridhishe kuwa maandamano hayo yatakayofanywa hayatakuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani.

Lakini pia umefika wakati kwa wananchi hasa vijana wanaoshajihishwa kuandamana kujiuliza je watakapofanya maandamano itakuwa ndio ufumbuzi wa kutatuliwa changamoto zao?

Kwa tunavyoelewa Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia inayofuata misingi ya sheria na utawala bora, kiasi kwamba wananchi wakiona kama kuna changamoto imeshindwa kupata majibu kwa njia ya mazungumzo, mfumo wa utawala umetuwekea mahakama.

Mahakama katika nchi ndicho chombo pekee cha kutoa haki kwa mtu anayedhani amethulumiwa ama amevunjia haki zake na kamwe haki haipatikani barabarani kwenye maandamano.

Kwanini tusitumie misingi ya utawala bora ili kupata haki kuliko kuhamasisha maandamano ambayo hatudhani kama yataweza kutuondoshea changamoto zilizopo.

Tungependa kuwaeleza vijana na wale wanaohamasishwa kushiriki kwenye maandamano kwamba unapovunja sheria utakumbana na walinda sheria na kwanini ukumbane na nguvu za walinda sheria?

Katika kundi la watu linaporushwa jiwe humfika yoyote, hebu fikiria likikupata wewe hao waliokuhamaisha uingie kwenye maandamano watakushughulikia, watajali maisha na maslahi yako, familia yako inayokutegemea itaendeshwa na nani.

Uchaguzi ni siku moja tu, maisha baada ya uchaguzi yatakuwepo na Zanzibar itakuwepo, lakini maendeleo ya nchi yetu yatategemea ulinzi wa amani tuliyonayo itakapovunja gharama za kuirejesha itakuwa kubwa.