NA NASRA MANZI

MPIRA wa miguu ni moja kati ya michezo inayopendwa zaidi duniani na mchezo pekee wenye ushindani zaidi kuliko michezo mingine.Mchezo huu pia umekua ukitoa ajira kwa walio wengi katika nchi zote duniani ikiwemo Tanzania bara na Tanzania visiwani.

Sote ni mashuhuda, nchi zote duniani ikiwemo Zanzibar, wapo walioziacha ajira zao za awali na badala yake kujiajiri katika mpira wa miguu .Kwa vile mchezo huu unachezwa katika ngazi Wilaya Mkoa hadi Taifa, ipo haja kwa uongozi unaoshughulikia mchezo huu, kuzitambua timu za madaraja ya chini ili mchezo huu kukua kwa kasi katika nchi yetu.

Timu hizi za madaraja ya chini zinamchango mkubwa sana katika kuibua vipaji na kutoa wachezaji wazuri, ambao baadae watapeperusha bendera ya nchi katika sehemu tofauti duniani.Kuinuliwa kimaendeleo timu hizi kutasaidia kuongozeka kwa uibuaji wa vipaji kwa wachezaji watakaokuwa na uwezo wa kuchezea klabu mbalimbali.

Imekuwa kawaida kwa timu hizi kuonekana haziuna umuhimu na thamani yake kuwa ndogo sana, na hata wakati mwengine kubezwa, kwa sababu ya kuonekana kuwa hazina ubora na  viwango.Tumesahau kuwa timu hizi ndio baba mlezi wa wachezaji ambao leo ni vioo vya taifa kiupande wa mchezo huu.

Mataifa mbalimbali duniani yameendelea kutokana kuwepo kwa mikakati ya kuendeleza mchezo huu, kwenye vijana na klabu za madaraja ya chini.

Na ndio maana wanafanikiwa na kutoa wachezaji bora duniani ambao huziingiza nchi zao kwenye historia nzuri kwa vizazi vijavyo kupitia mchezo wa mpira wa miguu.

Hivyo umefika wakati wa kujitathmini na kujichunguza ili na sisi tuweze kufikia walipofika wenzetu, huku tukiangalia sehemu gani ambayo tumekosea ambapo hadi leo tunashindwa kupata mafanikio.

Kudharauliwa kwa timu daraja ya tatu na kwenda chini ngazi ya wilaya imekuwa changamoto kubwa inayozuia maendeleo ya soka visiwani.Wachezaji na makocha  wa timu hizi wamekuwa mstari wa mbele na kupoteza muda wao kushughulikia timu zao.

Lakini hali mbaya ya maisha ya wachezaji  na viongozi wa timu hizo, inasababisha ugumu wa kuimarika mchezo huu.

Hii ni kwa sababu mchezaji ina mlazimu kutafuta mahitaji ya kifamilia kwanza badala ya kwenda kujumuika na wenzake kufanya mazoezi.Jambo hili linaonyesha wazi kuwa timu hizi hazina uwezo wa kujikimu mahitaji yao.

Hivyo ingependeza zaidi kwa uongozi wa mchezo huu kuweka mipango maalum itakayoweza kuziinua timu za madaraja yote.Pia kutoa fursa kwa timu za madaraja yote ili ziweze kuleta maendeleo ya kasi ya mchezo wa mpira wa miguu.