KATIKA dunia ya sasa suala la uhamiaji limekuwa tete na kwamba hata sababu za kutokea kwa wimbi kubwa la wahamiaji ulimwenguni zinaweza kukushangaza.

Dunia inakabiliwa na tatizo kubwa la uhamiaji ambalo linatokana na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanaadamu kukimbia majanga ya kibinaadamu mafuruko, matetemeko ya ardhi, vile vita, machafuko na ghasia nakadhalika.

Uhamiaji duniani pia unachangiwa na wanadamu kukimbia hali ngumu za kimaisha (umasikini), katika maeneo waliyopo na kuhamia katika maeneo ambayo wataweza kuishi vizuri.

Katika makala haya nataka tu tuangalie kwa hivi sasa nchi gani inayoongoza duniani kuwa na wahamiaji wengi zaidi.

Kwa mjibu wa mtaalamu wa masuala ya idadi ya watu, Gilles Pison alibainisha kuwa asilimia nne ya watu wote duniani wanaishi katika nchi ambazo hawakuzaliwa.

“Kumekua na mazungumzo mengi kuhusu wimbi la uhamiaji, lakini idadi inaonesha hadithi nyingine tofauti”, alisema Gilles Pison.

Moja kati ya mahitimisho la Pison katika utafiti wake ni kuwa mtazamo kuhusu uhamiaji unaweza kutofautiana kwa kiasi kikubwa kutokana na taarifa zinazopatikana kuhusu idadi ya watu wanaohamia.

Alitoa mfano wa kile kilichoitwa wimbi la uhamiaji Ulaya lililoanza mwaka mwaka 2015, ambalo lilisababishwa na ukosefu wa utulivu katika nchi za mashariki ya kati kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2017, nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E), ndiyo inaoongoza kuwa na asilimia kubwa ya wahamiaji ambapo ina asilimia 88.4 ya watu ambao hawakuzaliwa nchini humo.

Singapore inashika nafasi ya pili, ambapo ina idadi ya asilimia 46 ya watu ambao wamo nchini humo lakini si wazaliwa kwa maana ni wahamiaji.

Saudi Arabia ina asilimia 37 ya idadi ya wahamiaji, ikifuatiwa na Uswisi yenye asilimia 29.6 ya wahamiaji ambapo Australia ina asilimia 28.8 ya wahamiaji.

Nchi nyengine ni Canada ambayo ina asilimia 21.5 ya wahamiaji, ikifuatiwa na Austria yenye asilimia 19 ya wahamiaji, Marekani      ina asilimia 15.1 ya wahamiaji na Ujerumani yenye asilimia 14.8 ya wahamiaji.

Nchi yengine kwenye orodha hiyo ni Uingereza yenye asiliamia 13.4 ya wahamiaji, Uhispania yenye asilimia ya 12.8 ya wahamiaji na Uholanzi yenye asilimia 12.1 ya wahamiaji.

“Pamoja na wingi wake hasusani barani Ulaya, wahamiaji walianza kuingia kwa wingi tangu mwaka 2015 kutokana na mizozo ya mashariki ya kati, bado mtazamo kuhusu uhamiaji kimataifa haujabadilika”, alisema Pison.

“Umoja wa mataifa unasema inakadiriwa kuwa kulikuwa na wahamiaji wanaokisiwa kuwa milioni 258 mwaka 2017, sawa na ailimia 3.4 idadi ndogo ikilinganishwa na idadi ya watu duniani”.

“Kiasi hiki kimeongezeka kiasi katika kipindi cha miongo kadhaa, miaka 30 iliyopita, mwaka 1990 ilikuwa asilimia 2.9 na mwaka 1965 ilikuwa asilimia 2.3 mabadiliko ni kidogo katika kipindi cha miaka 100”, alisema.

Ulaya ina nchi tatu ambazo ziko kwenye nafasi kumi za kwanza zenye idadi kubwa ya wahamiaji ambazo ni Uswisi, Uingereza na Uhispania, hata hivyo, Uhispania ndiyo nchi mpya ambayo wahamiaji huingia kwa wingi.

“Uhispania ilikua nchi iliyokua na wahamaji mpaka mwishoni mwa miaka ya 1980, lakini sasa ina takriban asilimia 13 ya watu wake ni wahamiaji, karibu sawa na Marekani”, alisema Pison.

Lakini vipi kwa nchi ambazo zinashuhudia watu wake wakihama na kwenda kuishi kama wahamiaji katika nchi nyengine?

Haitashtusha kuiona India ikiongoza kwa idadi kubwa ya watu wake kuishi nje ya nchi, ambapo watu takribani milioni 16 wanaishi nje ya India zaidi kidogo ya asilimia moja (1%) ya idadi ya watu nchini humo.

Nchi inayofuata ni Mexico, yenye jumla ya milioni 12.5 wanaoishi nje ya nchi hiyo, ambapo kwa takwimu hizo inaonesha kuwa katika kila raia 10 wa Mexico, mmoja anaishi nje ya nchi hiyo.

Idadi ya nchi zinazoongoza watu wake kuishi kama wahamiaji katika nchi nyengine kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, India inaongoza ambapo raia wake milioni 16.6 wanaishi nje ya nchi hiyo.

Mexico inafuata ikiwa na watu wake takriban milioni 13 wanaishi nje ya nchi hiyo ikifuatiwa na Urusi ambapo wananchi wake milioni 10.6 wanaishi kama wahamiaji katika nchi nyengine.

China ina raia wake takriban milioni 10 wanaoishi nje ya nchi hiyo kama wahamiaji, ikifuata Bangladesh watu wake milioni 7.5, ahalafu Syria watu wake milioni 6.9 wanaishi kama wahamiaji katika nchi nyengine.

Pakistan nayo ina watu wake milioni 6 wanaoshi nje, ikifuatiwa na Ukraine raia wake     milioni 5.9, Ufilipino milioni 5.7, Uingereza milioni 4.9 na Afghanistanmilioni 4.8.

Uhamiaji ni mada inayogusa nchi nyingi duniani na kumekua na hofu kuhusu suala hilo huku katika baadhi ya nchi likichukuliwa kama ajenda muhimu ya kisiasa.

Utafiti wa Pison pia unabainisha nchi ambazo zina sifa ya kutoa na kupokea wahamiaji, mfano ni Uingereza, ambayo suala la uhamiaji limekua kwenye ajenda za kisiasa, na zimechukua nafasi kubwa kwenye maamuzi ya nchi hiyo katika kupiga kura katika kuondoka kwenye umoja wa Ulaya.