BERLIN,UJERUMANI
SHUGHULI za uchukuzi zimesimama katika miji kadhaa ya Ujerumani mapema baada ya wafanyakazi wa mabasi na treni kufanya mgomo ili kushinikiza kuwepo kwa sheria za ajira zinazofanana nchi nzima.
Uchukuzi umesimama katika miji ya Berlin, Hamburg, Hanover, Magdeburg, Kiel na Erfurt.
Aidha wafanyakazi katika sekta ya uchukuzi wa umma katika miji ya Munich, Constance na Freiburg pia wanapanga kushiriki mgomo huo.
Kampuni za uchukuzi zimewataka wateja wao kutafuta njia mbadala ya usafiri.
Katika eneo la Mecklenburg-Vorpommern, wanafunzi waliruhusiwa kutokwenda skuli iwapo usafiri wa umma hautakuwepo kwa sababu ya mgomo.
Chama cha wafanyakazi cha Verdi kiliitisha mgomo huo kushinikiza makubaliano ya pamoja kwa wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi wapatao 87,000.
Waajiri hadi sasa wamekataa kukubali sheria za kazi zinazofanana nchi nzima ambazo zitaondoa mfumo ulioko sasa ambao kila jimbo linaonekana kuwa na kanuni zake za kazi.