ROMA, ITALIA

MUUNGANO wa mashirika na jumuiya za kiuchumi za Italia umesema uchumi wa nchi hiyo umeporomoka vibaya na umerejea katika hali uliyokuwa nayo miaka 20 iliyopita.

Shirika la habari la IRIB limenukuu taarifa ya muungano huo ikisema kuwa,uzalishaji ghafi ndani ya Italia ulirejea kwenye kiwango cha mwaka 2000.

Taarifa ya muungano huo ilisema kuwa,harakati hiyo inayozidi kurudi nyuma inatokana na machaguo yasiyo sahihi ya Serikali zilizotawala Italia katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na kukosekana siasa na sera za kiviwanda nchini humo.

Muungano huo wa mashirika na jumuiya za kiuchumi za Italia ulisema pia kuwa,hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2020, uzalishaji ghafi wa ndani ya Italia utapungua kwa asilimia 12.

Watu 35,483 wameshapoteza maisha kutokana na ugonjwa wa corona nchini Italia hadi hivi sasa na zaidi ya 269,214 walithibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari.

Katika upeo wa bara Ulaya, Italia ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa COVID-19 baada ya Uingereza ambayo ndiyo inayoshika nafasi ya kwanza kwa vifo vingi vya corona barani Ulaya.