NA ZAINAB ATUPAE

VIONGOZI wa Siasa Nchini wameombwa kutangaza Siasa zao kwa kuhubiri Amani ambayo italinda Nchi katika kipindi hichi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

Akitoa ombi hilo huko Ofisi za Chama Cha UDP iliopo Mahonda, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Juma Khamis Faki,alisema bila ya amani hakuna jambo ambalo litafanyika kwa amani.

Alisema karibu na uchaguzi kuna baadhi ya watu wanaotumwa kwa makusudi kuharibu amani kwa kuleta sitofahamu kwa wananchi na chama.

Alisema sio vyema kufanya hivyo kwani nchi sio ya mtu mmoja au Chama fulani,hivyo ni vyema kila mmoja kuelezea Sera zake ambazo zitamsaidia kupata kura zitaweza kumpa nafasi ya kuongoza nchi au jimbo lake.

“Tufahamu kuwa hii Nchi si yachama Fulani tunatakiwa kutambua nchi yetu sote na kila mmoja anahaki ya kuchagua chama anachokita tunachotakiwa kuanzia viongozi na wananchi kuwa walinzi ambao tutaleta amani katika kipindi chote cha uchaguzi”alisema.

Alifahamisha kuwa kazi ya viongozi ni kunadi sera zao ambazo zitawavutia wananchi na kukubali kuwapa kura zao kwa lengo la kuleta maendeleo na mabadiliko ya nchi yao.

“Sio vyema Kiongozi kukaa mbele ya wajumbe kutoa sera mbaya au kukiponda chama hasa cha Mapinduzi kwa lengo la kukichafua kwa wananchi na kuonekana kibaya”alisema.

Aidha alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua wote ambao watajaribu kuhatarisha amani ya nchi yao kwa kutoa maneno machafu ambayo yatasababisha migogoro kati ya chama na chama.

Akizungumzia juu ya chama chake,alisema kuwa anazimini sana tume mbili za Uchaguzi,ikiwemo ZEC na NEC,hivyo alivitaka vyombo hivyo kutoa taarifa kwa mujibu wa matokeo yalivyo.