PARIS,UFARANSA

MAHAKAMA moja ya Ufaransa imeanzisha uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na benki moja ya nchi hiyo nchini Sudan.

Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu lilitangaza kwamba mashirika yasiyo ya serikali mwezi uliopita wa Agosti yalifanikiwa kufungua faili la uchunguzi dhidi ya Benki ya BNP Paribas ya Ufaransa na kushiriki kwake katika kufanya jinai dhidi ya binadamu nchini Sudan.

Ripoti zinasema kuwa, faili la kesi hiyo lilifunguliwa tarehe 26 mwezi uliopita wa Agosti katika mahakama ya Paris, yapata mwaka mmoja baada ya kutolewa mashitaka ya kushiriki benki hiyo katika kutenda jinai dhidi ya binadamu, mauaji, kutesa na kufanya ukatili dhidi ya raia wa Sudan.

Jumuiya ya Haki za Binadamu na wanaharakati tisa wa Kisudani waliokimbilia nje ya nchi ndio waliowasilisha mashitaka hayo. 

Benki ya BNP Paribas ya Ufaransa pia iliwahi kutuhumiwa kwamba ilishiriki katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Karibu watu milioni moja waliuawa katika mauaji hayo yaliyofanywa na Wahutu wenye misimamo mikali dhidi ya watu wa kabila la Tutsi.  

Benki ya BNP Paribas inatuhumiwa kuhusika na jinai zilizofanyika mwaka 2002 na 2008 katika eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa karibu watu laki tatu waliuawa huko Darfur na wengine karibu milioni tatu walilazimishwa kuwa wakimbizi.