TANGU chama tawala nchini Msumbiji cha FRELIMO na waasi RENAMO walipotia saini mkataba wa amani na kukomesha vita mwaka 1992, wananchi wa taifa hilo wamepata ahuweni kubwa.

Vita baina ya FRELIMO na RENAMO vilisababisha umwagikaji wa damu mkubwa na wa muda mrefu, ambapo utata ulianza pale wakoloni wa kireno walipoondoa nchini humo.

Tunaweza kusema kwamba tangu mwaka 1992, nchi hiyo imefurahia amani na kwamba tumeshuhudiwa chaguzi za kisiasa zinavyofanywa nchini humo zimekuwa za amani.

Hata hivyo, baina yam waka 2018 hadi 2019 nchi hiyo ikaelezwa kuwa imekuwa maficho ya wanagambo wa kiislamu wenye mafungamano na kundi la dola la kiislamu.

Marekani kama taifa lenye kupamabana na ugaidi likatahadharisha kuwa makundi ya wanamgambo yafanya operesheni nchini humo katika eneo la Kaskazini la Cabo Delgado, huku yakiungwa mkono na wanamgambo wa dola la kiislamu.

Wanamgambo hao wamekuwa wakishambulia vijiji mbalimbali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kusababisha vifo vya watu wasio na hatia.

Mkuu wa operesheni maalum ya Marekani barani Afrika meja Jenerali Dagvin Anderson, alisema kuwa kundi hilo limekuwa likipata msaada kutoka nje, hali inayolifanya kuwa hatari zaidi.

“’Tumewashuhudia wakiimarisha uwezo wao wa mashambulizi na kutumia mbinu ambazo hutumika pia katika maeneo mengine ya ulimwengu, ambako kuna makundi yenye uhusiano na Islamic State”, alisema jenerali Anderson.

Uasi wa wanamgambo wa kiislamu waliojitokeza nchini Msumbiji umegeuka kuwa vita vya wazi katika na kuna ripoti za mauaji ya watu, kukatwa kichwa na kutekwa nyara kwa miji miwili katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

Picha ya video, iliyopigwa mwezi Aprili mwaka 2020 kwa simu ya mkononi wilaya ya Muidumbe ulikuwa ushahidi wenye nguvu kuwa mzozo uliokuwa gizani katika eneo la Kaskazini mwa Msumbiji sasa umekuwa katika eneo la wazi kabisa kwa namna ambayo ni ya hatari.

Picha hizo za video zilipigwa katika eneo la bandari Mocimboa da Praia, ambalo lilidhibitiwa kwa muda na wanamgambo Machi 24 mwaka huu, siku mbili baadae, wanamgambo hao walidhibiti mji mwingine muhimu wa Quissanga.

“Sasa wana silaha na gari, zinazowafanya waweze kutembea kirahisi na kufanya mashambulizi kwenye eneo kubwa. Na hutumia sare za wanajeshi. Hivyo, watu huchanganyikiwa na kuogopa”, alisema askofu wa kikatoliki wa Pemba, Luiz Fernando Lisboa.

Kundi hilo lilitumia miaka miwili kutekeleza operesheni zao mafichoni, likivishambulia vijiji vya mbali, ikishambulia misafara ya kijeshi iliyo kwenye doria kwenye barabara, vitendo vya kigaidi dhidi ya jamii za vijijini.

Kwa ufupi katika kipindi cha miaka miwili inasemakana kiasi cha watu 200,000 wameyakimbia makazi yao, kukwepa kuuawa na waasi hao.

IS imedai kuhusika na mfululizo wa mashambulizi nchini Msumbiji, nchi ambayo asilimia 18 ya raia wa nchi hiyo ni waislamu na linaonekana kuhamasisha operesheni zake ambazo zimekuwa zikiweka alama zake katika maeneo kadhaa barani Afrika.

Wafuatiliaji wa mambo wanasema kuwa kuanza kwa uasi nchini Msumbiji ni sawa na operesheni za uasi za kundi la Boko Haram Kaskazini mwa Nigeria, kikundi ambacho kimekuwa kikitekeleza vitendo vya kigaidi dhidi ya jamii nyingi nchini humo, lakini pia imekuwa chaguo mbadala la vijana wasio na ajira na waliochanganywa na namna hali ya mwenendo mbaya wa maisha na mifumo ya kifisadi.

”Kwa mara ya kwanza walizungumza na Umma,” alisema mwanahistoria nchini Msumbiji, Prof. Yusuph Adam, ambaye amesema kuwa video hizo ziliipa ujazo hoja kuwa mgogoro wa Cabo Delgado umechochewa zaidi na masuala ya ndani.

”Jeshi tangu awali …lilikuwa likiwapiga watu, kuwafunga, kuwatesa. Kuna hofu miongoni mwa waislamu waishio eneo hilo. Wanatengwa kwa kuwa watu wanawafikiria kuwa wajinga.

”Tatizo ni kuwa kuna kundi la vijana wasio na ajira. Ikiwa tutatatua …matumizi ya nguvu, rushwa, na ikiwa tutakuwa na mfumo thabiti wa haki nina uhakika tutatatua shida hii haraka,” amesema Profesa Adam.

Hapo awali serikali ya Msumbiji ilitaka kupunguza uasi huo na kuwaondoa wanamgambo kwa makosa ya uhalifu na kuwazuia waandishi wa habari kuingia katika mkoa huo. Lakini hali hiyo inabadilika.

Baadaye, serikali ilianza kuajiri maafisa wa usalama wa kigeni – inadaiwa kutoka Urusi, Marekani na Afrika Kusini – kusaidia jeshi kumaliza uasi, lakini bila mafanikio yoyote makubwa.

Eneo lililovamiwa liko karibu na miradi ya utafutaji wa gesi asili yenye thamani ya dola bilioni 60 na ulilengwa mara kadhaa na wanamgambo mwaka huu, kabla ya Msumbiji kutwaa tena bandari hiyo.

Makampuni ya gesi- yamesitisha kuwekeza mabilioni ya fedha katika maeneo ya pwani ya Cabo Delgado – moja ni kwa sababu ya kukosekana kwa hali ya usalama, lakini pia kuporomoka kwa bei ya gesi.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, suluhu ya mgogoro itategemea utawala mzuri na uwazi katika masuala ya uchumi, usawa katika umiliki ardhi, ajira na mgawanyo sawa wa mapato yatokanayo na gesi.

”Makampuni ya kimataifa yanataka kujua kama wanaweza kuchukua hisa zao, lakini wanapaswa kuwaangalia wakazi wa eneo hili,” alisema askofu wa Pemba.

”Na serikali inapaswa kufahamu kuwa ni muhimu sana kuwa rasilimali hii lazima iwanufaishe watu na isiwe chanzo cha vitendo vya rushwa,” aliongeza.

Kampuni ya mafuta ya Ufaransa Total, ambayo inawekeza dola bilioni 23 katika mradi wa uchimbaji wa gesi ilisema kwamba haitegemei tena bandari ya Mocimboa da Praia kama eneo la kimkakati na kwamba sasa imejenga vifaa vyake baharini.

Taarifa za karibuni zinaeleza kuwa waasi bado wana nguvu kwani wameripotiwa kuviteka visiwa viwili vidogo vya bahari hindi na kutishia usafiri wa baharini katika eneo hilo ambapo mradi wa gesi yenye thamani ya mabilioni ya madola unajengwa.