KAMPALA,UGANDA

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda ametangaza kuwa, skuli na taasisi nyengine za elimu ya juu, zitafunguliwa tena kuanzia mwezi ujao wa Oktoba tangu zilipofungwa Machi mwaka huu.

Hatua hiyo inakuja wakati Uganda sasa imerikodi visa 6,287 vya maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki hukuu idadi ya vifo vya corona nchini humo ikifikia 63.

Hata hivyo ni wanafunzi Milioni 1.2 tu walioko kwenye madarasa ya mwisho ya kufanya mitihani ndio watakaoruhusiwa kurejea tena skuli, baada ya Serikali nchini humo kuregeza zaidi masharti ya kupambana na janga la Corona. 

Rais yoweri Museveni alisema kuwa, wanafunzi hao watarejea skuli kuanzia tarehe 15  ya mwezi ujao wa Oktoba, na kwamba, mikakati imewekwa kuhakikisha kuwa wanakuwa salama.

Tangazo hilo la Rais Museveni limekuja baada ya wadau mbalimbali wa sekta ya elimu nchini Uganda kulalamikia kimya cha Rais huyo kuhusiana na hatima ya kufunguliwa skuli nchini humo.

Wakati huo huo, Marekani imeendelea kuwa nchi ya kwanza duniani iliyoathiriwa vibaya na virusi vya corona ambapo hadi sasa zaidi ya watu milioni saba wameambukizwa virusi hivyo huku 204,118 wakipoteza maisha.

India inaifuatia Marekani baada ya kusajili kesi karibu milioni tano na nusu za maambukizo ya corona na vifo karibu laki moja hadi sasa.

Brazil, Russia na Peru zinafuata kwa kushika nafasi ya tatu, ya nne na ya tano duniani.

Barani Afrika nchi ya Afrika Kusini ndio iliyoathiriwa zaidi na virusi vya corona ambapo zaidi ya watu laki sita na 60 elfu wameambukizwa virusi hivyo huku watu karibu 16,000 wakiwa wamefariki dunia kwa Coviod-19.