ATHENS,UGIRIKI

UGIRIKI  imefungua kambi ya hema yenye uwezo wa kuwahifadhi wahamiaji 3,000 walioachwa bila makaazi baada ya moto kuiteketeza kambi yao ya Moria.

Hata hivyo ni mamia tu ya wakimbizi waliokubali kuingia katika kambi hiyo mpya.

Ugiriki inasema wakimbizi wote wanaolala nje watapatiwa sehemu mpya za kuishi katika muda usiozidi wiki moja.

Hayo aliyasema Waziri wa Uhamiaji wa Ugiriki Notis Mitarachi katika mkutano na waandishi wa habari , akisisitiza kuwa kila mhamiaji atakuwa na nafasi ndani ya kambi mpya.

Wakimbizi walio wengi wanalalamikia hali ilivyo katika kambi hizo za visiwa vya Ugiriki wakidai hifadhi kwenye nchi nyengine za Umoja wa Ulaya, au kuboreshewa maisha katika kambi hizo.

Mwandishi wa DW katika kisiwa cha Lesbos anasema kabla ya kuingia katika kambi hiyo mpya, wakimbizi hulazimika kuchukuliwa vipimo vya virusi vya corona.