ATHENS,UGIRIKI

SERIKALI  ya Ugiriki imewashutumu wahamiaji kuichoma moto kwa makusudi kambi yao ya Moria mnamo Septemba 8.

Moto huo uliteketeza makaazi ya wakimbizi wapatao 12,000 na kuwaacha maelfu bila mahali pa kuishi, wakiwemo watoto na wanawake wajawazito.

Msemaji wa Serikali ya mjini Athens Stelios Petsas aliwaambia waandishi wa habari, kuwa baadhi ya wakimbizi waliichoma moto kambi yao, ili kuishinikiza Ugiriki iwaruhusu kutoka visiwani na kwenda Ulaya .

Wiki iliyopita,Waziri wa uhamiaji wa Ugiriki alitoa madai kama hayo, hata kabla ya kukamilika kwa uchunguzi ili kufahamu chanzo cha moto huo.

Ugiriki ilikuwa ikijenga kambi mpya kwa ajili ya wakimbizi hao karibu na kijiji cha Panagiouda, lakini wahamiaji wengi hawana shauku ya kuingia katika makaazi hayo ya mahema meupe, wakihofia kusahaulika.