BERLIN,UJERUMANI
WAZIRI wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amekataa madai ya Urusi kuwa Ujerumani ilikuwa inachelewesha uchunguzi kuhusu kesi ya mkosoaji mkuu wa Serikali ya Urusi Alexei Navalny, ambaye anapatiwa matibabu baada ya kupewa sumu katika hospitali mjini Berlin.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni ya taifa cha ARD, Maas alisema kuwa Ujerumani tayari ilithibitisha itaidhinisha ombi la Urusi kwa ajili ya msaada wa kisheria kuhusiana na suala hilo na imekwisha wasiliana na balozi ya Urusi kuhusu suala hilo.
Maas alisema hakuna sababu ya kutokubali hilo. Maria Zakharova msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi , alisema serikali ya nchi hiyo itashirikiana na serikali ya mjini Berlin katika uchunguzi, lakini pia aliwashutumu maofisa wa Ujerumani kwa uchelewesho.