BERLIN,UJERUMANI

UJERUMANI  imesema itawapokea wakimbizi 1553 kutoka kambi za nchini Ugiriki, pamoja na watoto 150 wasio na familia,baada ya kambi yao ya Moria kuungua moto kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos usiku wa Septemba 8.

Baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zililazimika kuishughulikia adha ya wakimbizi hao, ambao wengi walikuwa wakilala mitaani na katika majengo yasiyokaliwa na watu kisiwani humo.

Naibu kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema nchi yake itazipokea pia familia zenye watoto ambazo tayari zimepewa hadhi ya ukimbizi nchini Ugiriki, hata kama zilikuwa haziishi katika kambi iliyoteketea.

Ufaransa ilikubali kuwapokea watoto 150, huku nchi kadhaa nyengine za Umoja wa Ulaya zikijitolea kuwapa hifadhi wakimbizi vijana wapatao 100 kutoka kambi ya Moria.

Moto mwengine ulitokea karibu na kambi ya Samos pia nchini Ugiriki, lakini maofisa walisema kambi hiyo yenye wakimbizi 4,700 iko salama.