BEIJING,CHINA

UMOJA  wa Ulaya umeihimiza China kuwaruhusu waangalizi huru kuingia katika jimbo lake la Xinjiang, ambako ripoti zinasema nchi hiyo inawafanyia ukandamizaji watu wa jamii ya wachache ya Waighur ambao ni Waislamu.

Katika mkutano wa kilele baina ya Ulaya na China uliofanyika kwa njia ya video, China pia ilitakiwa kujitolea kuachana na baadhi ya masharti yake, ili iweze kufikia makubaliano ya uwekezaji na Umoja wa Ulaya.

Siku za nyuma China ilikataa miito ya kuitaka iwaruhusu wachunguzi hao katika jimbo lake la Xinjiang lenye utajiri wa raslimali.

Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel ambaye alishiriki mazungumzo hayo yaliyomjumuisha pia rais wa China Xi Jinping, alisema Ulaya vile vile ilielezea wasiwasi wake juu ya sheria ya usalama wa taifa ya China kisiwani Hong Kong, ambayo aliitaja kuhujumu maadili ya kihistoria ya uhuru katika mji huo.