MADRID,UHISPANIA

BARA la Ulaya linapambana na ongezeko jipya la maambukizi ya virusi vya corona.

Nchini Uhispania ambako maambukizi mapya ya siku yaliongezeka hadi zaidi ya 4,000, mamlaka zilifunga baadhi ya maeneo ndani na jirani na jiji kuu la nchi hiyo, Madrid.

Polisi waliweka maeneo ya ukaguzi karibu 60 barabarani katika maeneo hayo, wakiwataka watu kuonesha vibali kabla ya kuingia au kutoka.

Kwa jumla,Uingereza ina idadi kubwa ya vifo vinavyohusiana na virusi hivyo barani Ulaya.Hivi karibuni, imeshuhudia maambukizi mapya zaidi ya 4,000 yaliyothibitishwa kwa siku.

Maofisa wa Serikali ya Uingereza walionya kwamba bila kuchukua hatua zaidi,nchi hiyo inaweza kushuhudia maambukizi mapya 50,000 kwa siku kufikia katikati ya mwezi Oktoba.

Waliongeza kuwa hali hiyo inaweza kumaanisha kutakuwa na vifo karibu zaidi ya 200 kwa siku mwezi mmoja baada ya hapo.

Waziri Mkuu Boris Johnson anazichunguza hatua mpya za kupambana na virusi hivyo.Anataka kuepuka ufungaji wa nchi nzima unaoweza kuathiri zaidi uchumi.

Kutokana na hofu ya ongezeko jipya la virusi hivyo, masoko ya hisa barani Ulaya yamekumbwa na wimbi la uuzaji hisa baada ya kufunguliwa .