NA MWANDISHI WETU

MAHARI ni hidaya inayotoka upande wa mume mtarajiwa na kwamba mahari huwa ni kitu chochote chenye makubaliano baina ya pande mbili ya mume na mke au hata wakati mwengine ni tamko la mke mtarajiwa.

Hata hivyo, kila jamii ina utaratibu wake wa kutoza mahari, ima iwe kwa taratibu za kidini kikabila au vinginevyo, ilimradi lile lengo la kutoa mahari hiyo inakuwa imefikiwa na muhusika baada ya kukubaliana na taratibu husika

Pengine ni vema tujiulize mahari ni nini? Na jamii inalichukuliaje suala hili hasa katika taratibu za wa maisha ya kila siku.

Kiujumla mahari ni aina ya malipo anayolipwa binti au malipo yanayotolewa na upande wa mume anayetaka kuoa kwa wazazi wa binti au bi harusi mtarajiwa.

Kwa sehemu kubwa malipo haya hutofautiana kati ya kabila moja hadi jingine na dini moja na nyengine.

Suala la mahari katika ndoa iwe kwa walioachana au waliomo katika ndoa ni muhimu sana na ni lazima kwa mujibu wa ndoa ya kiislamu.

Kama tunavyojua hapa Zanzibar asilimia kubwa ya watu wake ni waislamu hivyo ndoa nyingi zinazofanyika zinaendana kwa utaratibu wa dini hiyo.

Aidha mahari kama inavyotajwa katika dini ya kislamu ni ‘Hidaya’ hivyo haipaswi kuchukuliwa kama mzaha ama kutolipwa kwa muhusika wa ndoa ya mwanamke bila ya ridhaa yake.

Kwa mukhtaza huo basi nataka kumaanisha kuwa watu wengi hususan wanawake hapa Zanzibar wamekuwa wakikosa haki yao ya mahari baada ya kuvunjika kwa ndoa.

Kufuatia wimbi kubwa la kuvunjika kwa ndoa linalochangiwa na mambo mbalimbali jambo ambalo limekuwa likichangia kuongeza idadi ya wajane walioachika na hata watoto wa mitaani kutokana na kukosa matunzo ya wazazi wa wawili.

Kwa kuwa suala la ndoa ni la makubaliano baina ya pande zote mbili ya mke na mume leo hii kwa nini wanandoa wafikishane mahakamani kwa ajili ya kudai mahari?.