Awamu ya Dk. Shein visiwa vitano vyafaidika na huduma ya umeme
Njau, Kokota kunufaika karibuni
NA HUSNA MOHAMMED
“AMA kwa hakika ni ukweli ule msemo usemao ada yamja hunena muungwana ni vitendo”. Msemo huu umesadifu kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, pale ambapo ametekeleza ilani ya CCM kwa vitendo.
Zanzibar ya leo kwa maana ya Unguja na Pemba inang’ara kila mahala si mashamba, si mjini wala visiwa vidogovidogo, kuunga na kutumia umeme ni kwa wananchi wenyewe tu hasa kwa kuwa huduma hiyo imeshasambaa maeneo yote.
Kama tunavyojua sasa uongozi wa miaka 10 wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano ndio huo unamalizika, huku sekta zote akizigusa kwa kuzipelekea maendeleo.
Makala haya maalumu itazungumzia namna nishati ya umeme ulivyoimarika na sio kukamilika kwani umeme ni karibu asilimia 99 umeshakamilika utekelezaji wake.
Taaswira hiyo njema ya mafanikio katika sekta ya nishati ya umeme ilioneshwa hivi karibuni wakati Rais Dk. Shein akivunja baraza la wawakilishi ambapo pamoja na mambo mengine, alisema kuwa Nishati ya umeme ni muhimu katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi na ustawi wa maendeleo ya wananchi wetu.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika awamu zake mbali mbali imefanya jitihada kadhaa za kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa na huduma za nishati za umeme za uhakika.
“Katika uongozi wa Awamu ya Saba, niliahidi kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na Awamu za Uongozi wa Serikali zilizotangulia katika kusambaza na kuwafikishia wananchi huduma hizi popote walipo”, alisema Rais Shein.
“Nnafuraha kueleza kuwa hadi sasa Serikali imeweza kuufikisha umeme katika shehia zote za Unguja na Pemba. Nishati hii inapatikana katika vijiji 2,882 kati ya vijiji 3,259 sawa na asilimia 88.43 vikiwemo vijiji 354 vilivyopatiwa umeme katika kipindi hiki”, aliongeza.
Sambamba na hilo, lakini Rais Shein alifurahishwa na juhudi ya kuvipatia umeme visiwa vidogo vidogo vitano vya Pemba.
Alivitaja visiwa hivyo kuwa ni pamoja na Kisiwa Panza, Makoongwe, Shamiani (Mwambe), Fundo na Uvinje.
Alisema Jitihada za kuufikisha umeme katika kisiwa cha Kokota na Njau huko Pemba zilipata changamoto na kusababisha kuchelewa kidogo.
Hata hivyo, alisema fedha kwa ajili ya kazi hio zimeshatengwa na utekelezaji wa mpango huo utaendelezwa kama alivyoahidi.
“Nawanasihi wakaazi wa kisiwa cha Kokota na Njau waendelee kuwa na subira, Mwenyezi Mungu atatujaalia dhamira yetu hii njema itafanikiwa. Naupongeza uongozi na wafanyakzi wa Shirika la ZECO pamoja na Wizara kwa kazi kubwa ya kusambaza umeme hapa Zanzibar”, alisema.
Aidha Rais Shein alisema kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme yaliyojitokeza pamoja na kupata msaada wa Kampuni ya MCC ya Marekani kwa kuunganishwa waya wa baharini wa Megawati 100, mwaka 2010,
“Serikali imeamua kuwa ipo haja ya kuwa na umeme wa uhakika na tayari ishaanza kutafuta njia mbadala za kupata vyanzo vipya vya nishati ya umeme.
Sambamba na hilo, alisema Utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) umeonesha kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa Zanzibar kupata nishati ya umeme kutokana na nishati ya jua.
Hivyo, alisema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo na limefikia hatua nzuri sana, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na sekta binafsi, ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa nishati hii.
“Tumeambiwa kuwa Benki ya Dunia itatuunga mkono kwa kuanzia kupata MW 35, lakini wapo wawekezaji walojiandaa kuwekeza zaidi ya MW 70 na kadhalika”, alisema Rais Dk. Shein.
WANANCHI WA VISIWA VILIVYOFAIDIKA NA NISHATI HIYO WANASEMAJE
FUNDO

“UMEME ulipokuwa haujafika kisiwani kwetu tulikuwa tukipata tabu sana kila kitu kilitulazimu kwenda Wete, lakini kwa sasa tunamshukuru sana Rais Shein kwa kutufikishia umeme hapa kisiwani kwetu Fundo.
Hayo ni maneno ya Riziki Said Abeid, Mkaazi wa kisiwa cha Fundo kilichoko Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Riziki alisema kwa sasa mambo yote yanayotaka huduma ya umeme wanafanya kisiwani kwao Fundo pasi na kufika mjini Wete.
“Hivi sasa tunachaji simu zetu, tunapikia makuka, tunahifadhi samaki wetu kwa kutumia mafriji, kuangalia televisheni, kupiga pasi nakadhalika”, alisema Riziki huku akionekana na shauku kubwa.
Nae Seif Said Abeid ambae kazi yake ni ya Uvuvi, alisema kuwa umeme umewaokoa sana watu wa Fundo hasa wavuvi.
“Ama hili alilolifanya Rais Shein ni kubwa sana kutupatia umeme watu wa visiwa, kwani umeme ni mambo yote hasa wakati huu wa sayansi na teknolojia mimi kama mvuvi hivi sasa sina wasiwasi nikirudi kuvua samaki wangu nawauza kama hawajesha nawaweka kwenye Friza”, alisema.
Aidha alisema kabla ya kufika umeme Fundo wanalazimika kwenda Wete kuhifadhi samaki kwa fedha nyingi jambo ambalo ni hasara kubwa.
“Tulikuwa tukipata hasara mara mbili kwanza ya kuhifadhi samaki, halafu kuchajiwa fedha lakini kwa sasa tukishanunuwa umeme wetu basi”, alisema Seif ambae kazi yake ni uvuvi.
Kwa upande wake Khatib Khamis Omar, mkaazi wa kisiwa hicho cha Fundo, ambae pia ni Mwalimu wa skuli ya Fundo, alisema kuwa kabla ya kupata umeme wakifuata huduma zote Wete jambo ambalo likiwasababishia usumbufu mkubwa.
“Kazi zetu za ofisi kama kuprinti karatasi, kuchaji simu, kupandisha maji kwenye matangi tulikuwa hatuna lakini kwa sasa huduma hizi tunazipata hapa skulini kwetu, hata kama tunataka kuwasaidia wanafunzi masomo ya ziada basi umeme wetu tunao skuli”, alisema.
Aidha Suleiman Amour, ambae ni mfanyabiashara ya duka kisiwani Fundo, alisema huduma ya umeme imekuwa ni muhimu sana kwao kwa kuwa wanafanyabiashara zao za kuuza duka hadi muda wanaotaka.
“Umeme ulipokuwa haujafika ikifika saa 11: 00 tunalazimika kufunga maduka lakini kwa sasa umeme upo tunauza maduka mpaka saa 5 usiku, tunachaji simu zetu hapahapa”, alisema.
MAKOONGWE
Kwa upande wa kisiwa cha Makoongwe wakazi wake wameisifu sana serikali ya awamu ya Saba kwa kuwaona wakaazi wa visiwa vidogovidogo.
“Tunashukuru uongozi wa awamu ya saba kwa kutuona kwani tulikuwa tunawaonea choyo wenzetu wa kisiwa cha Kojani au tukienda mjini kama Mkoani tukiona umeme tunaona choyo lakini leo umefika ni hatua kubwa tunamshukuru Rais Shein”, alisema Roda Dhamir Kombo.
Roda ambae ni mwanamama anaevua chaza kisiwani Makoongwe, alisema kuwa kabla ya kufika umeme alilazimika kuwachemsha chaza wake na kuwakausha lakini kwa sasa anawaweka kwenye friza.
“Mimi kazi yangu ni kuvua chaza, tena mwenyewe nawakausha nauza mkoani kwa wasafiri au wakati mwengine nasafirisha nje ya Pemba, hivi sasa Napata tija ukilinganisha na kabla ya kufika umeme”, alisema Roda.
Nae Khamis Said Maosud ambae ni mfanyabiashara wa vitu mbalimbali alisema anauza vitu vibaridi kama juisi, soda na bidhaa nyengine ambapo kwa sasa alisema biashara yake imekuwa mara dufu.
Kwa upande wake mkaazi mwengine wa kisiwa hicho cha Makoongwe, aliejitambulisha kwa jina la Haji alisema kabla ya umeme kisiwani kwao walilazimika kwenda Mkoaani mjini kuchaji simu na kufanya vitu vyengine lakini kwa sasa huduma zote wanazipata mjini.
KISIWA PANZA
Mkaazi wa kisiwapanza Mwanakombo Kae, alisema kila siku alilazimika kutumia mafuta ya taa zaidi ya shilingi 2,000 lakini kwa sasa mwezi mzima anaweza kutumia shilingi 5,000 na kama matumizi yatakuwa makubwa anatumia kama shilingi 10,000 lakini bado si hasara kwa kuwa ukipanga 2000 kwa siku kwa mwezi zinapita shilingi 10,000.
“Ukali wa maisha ulituandama sana wakaazi wa visiwa vidogovidogo lakini kwa sasa maisha magumu mtu kujitakia yeye mwenyewe”, alisema Mwanakombo.
Aidha Mzee Ali Kae ambae ni mvuvi alisema ameweza kujinunulia friza la kuhifadhia samaki yeye mwenyewe na sasa faida yake anaiona.
“Hapa kisiwani hakuna asiejua kama uvuvi ndio maisha yetu, kwa kuwa sasa hatuendi tena Mkoani kuhifadhi samaki tunauza hapa na tunawahifadhi hapa, Rais Shein tunampongeza kwa kuona umuhimu wetu watu wa visiwani”, alisema.
Nae Mwajuma Faki, ambae ni mfanyabiashara wa vitu vikavu kama vileja, keki na vitu vyengine alisema kwa sasa anamiliki jiko lake la kuka na biashara yake inakwenda vizuri sana.
Visiwa kama vile Makoongwe, Kisiwa Panza, Fundo, Uvinje na Mwambe Shamiani vimeweza kupatiwa umeme na Serikali bila kuangalia idadi ya watu wanaoishi katika visiwa hivyo au itikadi za kisiasa za watu wake.
Awali Visiwa ambavyo havijawahi kutumia nishati ya umeme lakini sasa ndani ya Awamu hii ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein, vimeweza kuipata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya kila nchi.
Waswahili wanasema Muungwana ni Vitendo na Dk. Shein ameonesha uungwana wake kwa kuahidi jambo na kulitekeleza ndani ya kipindi kifupi tu na sasa wananchi wa visiwa hivyo wanafaidika na huduma ya umeme kama maeneo mengine ya Zanzibar.
Serikali imeweza kutumia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kufikisha umeme katika visiwa hivyo vidogo vidogo kwa lengo la kuinua hali za kimaisha na kiuchumi kwa wananchi wake.
Visiwa vyengine vilivyobakia vya Kokota na Njau ambavyo Serikali imeahidi kuvisambazia umeme navyo vitafaidika na huduma hiyo muda sio mrefu kwa sababu matayarisho ya kazi hiyo yameshakamilika na kilichobakia kukaa mkao wa kula tu kwa wakazi wa visiwa hivyo.
Kinachofurahisha na kutia moyo kuona kazi zote za usambazaji umeme vijijini na visiwa vidogo vidogo zimefanywa na wataalamu na watendaji wetu wazalendo kupitia Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na hikvyo kuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwalipa washauri wa kazi hizo.
Visiwa ambavyo Serikali ilisambaza umeme kwa kushirikiana na wafadhili wa maendeleo ni Kojani, Tumbatu na Uzi Ng’ambwa katika awamu zilizopita za uongozi.
MENEJA MAWASILIANO ZECO
Akizungumza na Makala haya, Meneja wa mawasiliano kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Salum Abdalla, kuhusiana na umuhimu wa nishati hiyo kwa visiwa vidogo vidogo vya Unguja na Pemba, alisema kuwa nishati hiyo sasa imefika karibu visiwa vyote.
“Ama suala hili la nishati rais Shein amelitekeleza vyema kwa kuwa umeme sasa unang’ara hadi katika visiwa vidogovidogo jambo ambalo linafaa kupongezwa sana”, alisema Salum.
Akifafanua zaidi meneja mawasiliano huyo, alisema serikali imeimarisha shughuli za usimamizi wa huduma za umeme na usambazaji wa nishati hiyo mijini na vijijini vikiwemo visiwa vidogo vidogo vinavyoishi watu.
Salum alisema kuwa nishati ya umeme katika visiwa vya Unguja na Pemba imesambazwa kwa zaidi ya asilimia 90.
“Serikali imeshaanza maandalizi ya upelekaji Umeme kwenye visiwa vya Kokota na Njau huko ambapo ndani ya mwaka huu tunatarajia vipate nishati hiyo na kutimiza lengo la ilani ya CCM na ahadi ya Rais Shein wakati akiingia madarakani”, alisema.
Alisema usambazaji wa umeme katika visiwa vyote vidogo umefanywa kupitia wataalamu wa ZECO.
Katika miaka hii 56 tokea Mapinduzi ya mwaka 1964 maendeleo makubwa yameweza kupatikana katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii. Lakini unapozungumzia maendeleo hayo huwezi kuyaacha nyuma maendeleo makubwa yaliopatikana katika sekta ya umeme.
Sekta hii ambayo ni msingi katika maendeleo ya taifa lolote lile duniani, imeweza kuenea katika kila shehia na na vijiji vikubwa vya Unguja na Pemba.
Kazi ya usambazaji umeme inayofanywa na Serikali kupitia Shirika lake la Umeme Zanzibar ZECO imeweza kukuna nyoyo za wananchi wengi baada ya kuikosa huduma hiyo tokea karne na karne.
Ahadi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha vijiji na visiwa vidogo vidogo vyote vya Unguja na Pemba vinafikishiwa huduma ya umeme. Kwa asilimia kubwa ahadi hiyo imetekelezwa kivitendo kwa vile visiwa vidogo vidogo vinane kati ya kumi vimeshapatiwa huduma ya umeme.
Cha kufurahisha zaidi kazi zote hizi za usambazaji umeme zinafanywa na wataalamu wazalendo kutoka Shirika la umeme na hivyo kuokoa mamilioni ya fedha ambayo ingetumika kukodi washauri kutoka nje kusimamia kazi hizo.
MENEJA MKUU ZECO
Akizungumzia hatua za maendeleo zilizofikiwa na Shirika hilo, Meneja Mkuu wa ZECO Hassan Ali Mbarouk, amesema kazi ya usambazaji umeme ni endelevu lakini hadi sasa mafanikio makubwa yameweza kupatikana kutokana na huduma hiyo kusambaa maeneo yote ya mjini na vijijini.
Alisema hivi sasa shehia zote za Unguja na Pemba zimefikishiwa huduma ya umeme na vijiji vyote vikubwa vina umeme isipokuwa vitongoji vichache na maeneo mapya yanayochipuka hivi sasa.
Meneja Mkuu huyo alifahamisha kuwa visiwa vidogo vidogo vinane vimeshapatiwa umeme Unguja na Pemba na visiwa viwili vilivyobakia vinatarajiwa kupatiwa huduma ya umeme ndani ya mwaka huu wa 2020.
Alisema kuwa kazi ya usambazaji umeme yote inafanywa na Serikali kupitia Shirika la Umeme na kwamba hivi sasa inaratibu maeneo mapya ya makazi na kilimo ili yaweze kuwekwa katika mpango kazi wake na kuyapelekea umeme.
Hassan aliongeza kuwa kuimarika kwa sekta ya umeme nchini kumesababisha maendeleo katika Nyanja nyengine za kiuchumi kama vile kilimo na Utalii.
Aidha meneja huyo aliahidi kuwa Serikali inakusudia ifikapo mwaka 2022 kuona vijiji vyote vilivyobakia vinafikishiwa umeme. Hata hivyo, alisema kasi ya uungaji umeme majumbani bado haijaridhisha kwa vile hadi sasa ni asilimia 55 tu kaya ndio zimeunganishiwa umeme.
“Katika kushajihisha wananchi kujiunganishia umeme ZECO imetoa fursa ya kuwapoesha wananchi kuwapa mkopo katika uungaji wa umeme ili kuongeza kasi ya wananchi waliojiunga na huduma hiyo,” alifahamisha.
“Serikali imefanya mambo makubwa sana katika upatikanaji wa umeme hasa kipindi cha miaka tisa ya uongozi wa Dk. Shein ambapo vijiji zaidi ya 500 sawa na asilimia 90, kutokana na ukuaji wa makaazi kumekuwa na maeneo mapya ya makaazi na vitongoji vidogo vidogo kazi inaendelea”, aliongeza.
Aidha meneja mkuu huyo alisema upatikanaji wa umeme umepungua sana na kila mkoa kuna vituo vya ufundi ili kuona kuwa hakuna matatizo ya ukatikaji wa umeme.
Ama kweli umeme ni maendeleo kwani yeyote atakaetembelea visiwa hivi ataona mabadiliko makubwa ya kimaisha na kiuchumi ya wananchi wa maeneo hayo kutokana na utumiaji wa nishati ya umeme ambayo kwao imelewaletea ukombozi.
Mafanikio makubwa yaliopatikana na ZECO katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya usambazaji Umeme vijijini na visiwa vidogo vidogo ni ushahidi wa kutosha kwamba Serikali imepania kikamilifu uleta Mapinduzi ya kweli ya kimaendeleo katika Sekta mbali mbali kama mengi tunayoshuhudia.
Hadi sasa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) limefanikiwa kusambaza umeme katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa asilimia 87 na kuifanya sehemu kubwa ya vijiji nchini kupata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo.
Nishati ya umeme ni muhimu katika nchi yoyote ile duniani kwa kuwa inaharakisha maendeleo hasa katika wakati huu wa matumizi ya sayansi na teknolojia.
Hivyo Zanzibar kama sehemu ya dunia nayo inatumia nishati ya umeme jambo ambalo linasaidia kuipatia mapato serikali kupitia huduma mbalimbali.