BEIRUT, LEBANON

UMOJA  wa Mataifa umetahadharisha kuhusu athari mbaya za uhabiribifu wa mazingira za mripuko uliotokea mwezi uliopita kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon.

Ofisa wa mazingira na nishati wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Lebanon aliwaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba,mbali na idadi ya watu waliofariki dunia, mripuko wa bandari ya Beirut utakuwa na athari nyengine mbaya za muda mrefu kwa mazingira.

Ofisa huyo wa Umoja wa Mataifa alisema,japokuwa uchafuzi mkubwa wa mazingira uliotokea baada ya mripuko huo umepungua lakini chembechembe za kemikali zilizosababishwa na mripuko huo zinaweza kubakia angani na kuwa na madhara kwa afya ya jamii.

Mripuko mkubwa uliotokea tarehe 4 Agosti katika bandari ya Beirut ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 190 na kujeruhi wengine karibu 6000.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mripuko huo ulisababisha hasara ya mabilioni ya dola za Marekani.

Nchi nyingi dunia ikiwemo Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran, zimetuma misaada ya hali na mali kwa ajili ya kuwasaidia watu waliopatwa na madhara kutokana na mripuko huo.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif sambamba na kuwasilisha salamu za rambirambi za Serikali na wananchi wa Iran kwa taifa na Serikali ya Lebanon.

Alisema Jamuhuri ya Kiislamu itaendelea kuwasaidia watu waliopatwa na maafa katika tukio la bandari ya Beirut na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kushiriki katika ujenzi mpya na ukarabati wa uharibifu na hasara zilizosababishwa na mripuko wa bandari ya Beirut.