TRIPOLI,LIBYA
BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kutekeleza vikwazo vya silaha dhidi ya Libya na kuondoka mamluki wote katika nchi hiyo ya Kiafrika.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio hilo kwa kura 13 za ndio.
China na Russia hazikulipigia kura azimio hilo,Baraza la Usalama aidha limesisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo ya kisiasa nchini Libya na kusitishwa mapigano ya ndani.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa walizituhumu pande zinazozozana nchini Libya na nchi zinazounga mkono vita nchini humo kwa kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa na kueleza kuwa,kufuatia misaada ya moja kwa moja ya Uturuki na Imarati,utumaji wa silaha wa nchi hizo huko Libya umeongeza hatua ambayo inakiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.