SANAA,YEMEN

BARAZA la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limelitaka Baraza la Usalama liwasilishe faili la Yemen katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake mjini Geneva Uswisi liliashiria ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

katika vita vinavyoendeshwa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen na kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liwasilishe ombi la Mahakama ya ICC ili kufuatilia hali ya Yemen.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa aidha limetaka kusitishwa utumaji silaha kwa muungano huo vamizi katika vita huko Yemen. 

Baraza hilo limesisitiza kuwa kitendo cha kuutumia silaha muungano vamizi wa Saudi Arabia unaoendesha vita huko Yemen kunaifanya hali ya mambo ya nchi hiyo kuwa mbaya zaidi.

Josep Borrell Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya pia alifanya mazungumzo na Faisal bin Farhan Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia huko Brussels na akabainisha wasiwasi wake kuhusu matukio yanayojiri Yemen na kuzitolea wito pande zinazozozana kuhitimisha mapigano nchini humo.

Itakumbukwa kuwa, Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyengine kadhaa zilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa anga, baharini na nchi kavu.

Mashambulizi hayo ya Saudia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa yameuwa Wayemeni zaidi ya elfu 16, kujeruhi makumi ya maelfu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya wengine.