GITEGA,BURUNDI

SHIRIKA la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) limesema bara la Afrika limepoteza zaidi ya dola bilioni 800 ndani ya miaka michache iliyopita kutokana na magendo na mzunguko haramu wa fedha.

Katika ripoti yake ya kila mwaka,UNCTAD ilisema fedha za mtaji zilizotoka nje ya bara hilo kinyume cha sheria katika kipindi cha miaka 15 iliyopita ni zaidi ya dola bilioni 830.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,kuanzia mwaka 2013 hadi 2015,magendo hayo ya fedha zinazopelekwa nje ya bara la Afrika kinyume cha sheria yaliongezeka hadi wastani wa dola bilioni 89 kwa mwaka.

Hii ni katika hali ambayo, nchi za bara hilo kwa wastani hupokea misaada na ufadhili wa dola bilioni 102 kwa mwaka kutoka nje ya bara hilo na baadhi ya fedha hizo huingizwa barani humo kwa njia ya uwekezaji wa moja kwa moja.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa ulisema kuwa, nchi za bara Afrika zinapoteza mabilioni ya dola katika magendo ya vito na madini ya thamani kama dhahabu, almasi na platinamu.

Mafisadi wanafanya magendo haya ili kukwepa kulipa kodi na wasifuatiliwe vyanzo vya mali na mapato yao, na kuliacha bara hilo likikosa huduma muhimu kama za afya, elimu na miundo mbinu.