NA KHAMISUU ABDALLAH                                  

Mkurugenzi Tume ya Ukimwi Zanzbar, Dk.Ahmed Mohammed Khatib ameitaka Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar (ZAPHA+) kuhakikisha msaada wa vifaa kinga waliopatiwa wanavitumia na kuwaifikia walengwa ili kujikinga na maradhi mbalimbali.

Kauli hiyo aliitoa katika hafla ya kukabidhiwa msaada wa vifaa hivyo ikiwemo sabuni na jiki na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Maradhi ya Ukimwi Duniani (UNAIDS) hafla ambayo ilifanyika katika ofisi za jumuiya hiyo Sebleni.

Alisema wananchi watambue kuwa bado maradhi ya corona yanaendelea kushumbua nchi nyingi duniani hivyo ni vyema kuendeleza jitihada za kujikinga na maradhi hayo yasizuke tena nchini.

“Tutambue kuwa hatutakiwi kujibweteka kwani maradhi haya yanayofanana na mfumo wa korona mara nyingi yanavyoingia yanakawaida ya kujirejea hivyo Tanzania tujitahidi kuona tunaendeleza usafi kama serikali inavyotusisitiza ili kuona tunayadhibiti kidhati na hayaingii tena,” alisisitiza.

Alifahamisha kwamba Tanzania ikiwemo Zanzibar, imeruhusu muingiliano wa watu kutoka nchi mbalimbali duniani hivyo ni lazima kila mmoja kuchukua jukumu la kujikinga na maradhi hayo.

Mkurugenzi Ahmed, alisema vifaa hivyo vitasaidia sana katika kujikinga na kuendelea kuchukua tahadhari kwani maradhi ya corona ambayo yanaendelea kuzitesa nchi mbalimbali duniani.

“Pamoja na Tanzania tuweza kudhibiti maradhi haya lakini bado majirani zetu yanaendelea kuwasumbua hivyo tuendelee kuchukua jitihada za kujikinga wakati wote,” alisema.

Akizungumzia maradhi ya Ukimwi, alisema lengo la serikali kupitia tume ya ukimwi Zanzibar ni kuhakikisha ikifikia mwaka 2020, iwe imefikia 90 tatu, ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanajitambua, asilimia hiyo ya wanaoishi na virusi wawe wameanzishiwa dawa, na asilimia 90 wawe virusi vyao vionekane vipo chini wale ambao tayari wameshanzishiwa dawa.

Hata hivyo, anasema lengo jengine ni kuona ikifika mwaka 2030 Zanzibar haina tena maambukizi mapya ya VVU, kwani tathmni ya mkutano wa nchi zilizokuwemo Kusini wa Afrika (SADEC) katika masuala ya ukimwi hasa kinga Zanzibar imeweza kufikia tisini mbili.