NA TATU MAKAME

SHIRIKA la umoja wa mataifa linaloshughulikia mipango na maendeleo (UNDP) limesema litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kusimamia mipango ya ndani iliyowekwa ili kuona inakamilika kwa wakati.

 Mwakilishi kutoka shirika hilo Kimwaga Muhidini alisema hayo wakati akizungumza na viongozi wa dini, masheha, taasisi za kiraia za Wilaya za Magharibi ‘A’ na ‘B ’kwenye mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uelewa juu ya maendeleo endelevu yaliyofanyika  katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Magharibi ‘B’ Kwa Mchina.

Alisema dunia imekuwa ikipanga mikakati ya kitaifa katika kufikia maendeleo ya uchumi ambapo na Zanzibar iliweka mikakati ya ndani katika kufikia maendeleo endelevu kupitia (MKUZA III) hivyo shirika hilo litakuwa bega kwa beka kuisaidia Zanzibar katika kufikia Malengo hayo.

Alisema Zanzibar iliweka mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini (MKUZA III) mnamo mwaka 2016 -2020 hivyo shirika hilo lipo tayari kusaidiana na serikali kuona mpango huo unakamilika kwa wakati.

Alieleza kuwa mpango huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kuleta maendeleo kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Kimwaga aliwataka wadau hao kuifikisha elimu hiyo kwa jamii ili wajue mipango inayopangwa na serikali juu ya mipango endelevu hasa mikakati ya ndani.

Wakichangia mada kuhusu kuanzishwa mpango huo   wadau kutoka Jumuiya ya maendeleo Kojani (KOFLO), Faki Othman Haji na masheha wa wilaya hizo waliitaka serikali kuliangalia kwa upana suala la uharibifu wa mazingira ya bahari hasa kwenye uvuvi wa kutumia zana za kijadi.

Walisema sehemu hiyo imekuwa ikiathirika kutokana na kuwepo kwa vijana ambao wanaendeleza shughuli za uvuvi bila kuwa na elimu hali inayopelekea kuongeza kiwango cha uharibifu wa mazingira hapa nchini.

Shufaa Abdalla Khamis kutoka Tume ya Mipango Zanzibar, alisema tume hiyo imekuwa na mikakati maalum kuhakikisha wananchi wote wanatekeleza malengo ya maendeleo endelevu yanayowekwa na serikali.