NA LAYLAT KHALFAN

SERIKALI ya Wilaya ya Kusini Unguja, imesema katika kipindi cha mwisho cha miaka mitano ya uongozi wa Dk.Shein, maendeleo  mbalimbali yameonekana wilayani humo ikiwemo kukua kwa elimu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Idrissa Kitwana Mustafa, aliyasema hayo ofisini kwake Makunduchi, wakati akizungumza na mwandishi wa habari wa Zanzibarleo

Alisema suala la elimu ndani ya wilaya yake limepiga hatua kubwa huku vijana wakiwa wanathamini zaidi masomo yao na kufaulu vyema mitihani yao.

Alisema hivi sasa skuli nyingi za wilaya hiyo zimejengwa na kukarabatiwa, maabara ya kisasa katika maeneo ya Bwejuu sambamba na kujengwa Chuo cha Amali ambacho kipo maeneo ya Kisongo Makunduchi kilichojengwa chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Kitwana alisema kwa upande wa madawati yapo mengi ambayo yanawahamasisha wanafunzi kufika skuli kwa wakati na kusoma kwa bidii.

Akizungumzia masuala ya Afya, Idrissa alisema ndani ya wilaya yake   wana hospitali kubwa ya wilaya iliyopunguza kasi ya wagonjwa wengi kupelekwa katika hospitali nyingine.

Alisema kupitia halmashauri yao walifanikiwa kupata hospitali mpya maeneo ya Paje ya mama wajawazito na watoto, kituo cha watoto njiti , nyumba za madaktari ambayo inavifaa tiba vya kisasa kwa kiwango cha miaka hii wanayokwenda nayo huku dawa zikiwa zinapatikana kwa wakati.