NA MWANDISHI WETU

HALI ya kumiliki ardhi kwa wanawake bado duni, licha ya kuwa asilimia kubwa ya rasilimali hiyo hutumiwa na wanawake hao.

Hali hiyo huchangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo mifumo iliyopo haijampa kipaumbele mwanammke kuona kwamba nae ni mtu muhimu wa kumiliki ardhi.

Kuendelea kwa hali hii kunaonekana bado juhudi za wanawake kufikia maendeleo ya dhati kwa ajili ya kuinua uchumi wao na kusimamaimara kama wao bado.

Hivyo kutokana na hali hiyo imewafanya wanaharakati tofauti kupaza sauti zao ili kuwasaidia wanawake kupata haki yao hiyo kwani ni muhimu kwa maisha yao.

Kwa mfano wadau wa maswala ya wanawake chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, inaelimisha jamii kwa lengo la kuwawekea misingi imara wanawake kuona kwamba uchumi wao unaimarika na kuwa na maendeleo bora kwa ajili yao na taifa kwa ujumla.

Kuanzia 2016 TAMWA ilianza jitihada za kuwahamasisha wanawake wa wilaya ya Kaskazini ‘A’ na ‘B’ pamoja na wilaya ya kati kupata hati hizo, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda ipasavyo.

Kipindi cha 2017/18 TAMWA iliwafikia zaidi ya wanawake 700, walijengewa uwezo juu ya umuhimu huo kati yao wanawake sita tu ndio waliyobahatika kupata hati miliki wengine 90 maombi yao yapo katika hatua mbalimbali za kupata hati hizo.

Mbali ya wadau hao kufanya hivyo, serikali nayo haipo nyuma katika kuunga mkono jitihada hizo pamoja na kuwasaidia wanawake kupata haki zao kutokana na umuhimu huo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Serikali ilifanya mambo mengi katika kusimamia suala hilo ikiwemo kuanzishwa kwa mahakama ya ardhi ili kuzifanya kesi zote zinazohusu masuala hayo kusikilizwa katika chombo maalum ili kuwasaidia wananchi wake.

Serikali pia imeanzisha kitengo maalum pamoja na utaratibu wakusajili ardhi ili kuondosha migogoro iliyokuwa ikitokea.

Aidha tume ya kurekebisha sheria imeanza kukusanya maoni kwa wananchi wa wilaya ya Chake Chake juu ya sheria ya umiliki wa ardhi namba 12 ya 1992 na sheria ya mahakama ya ardhi namba saba ya mwaka 1994.

Tume hiyo imefanya hivyo baada ya kubaini kwamba Zanzibar inasheria nyingi za zamani ambazo zimekuwa kikwazo kidogo katika kuwasaidia wananchi, hivyo kufanyiwa marekebisho hayo zitasaidia kuendana na wakati uliyopo pamoja na kuleta tija kwa jamii hususani wanawake.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2017/18, umeonesha kwamba wanawake wanaomiliki ardhi ni asilimia 20 hadi 25, ambapo idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na asilimia ya wanawake wote waliyopo katika visiwa hivi.

Ardhi ndio kila kitu katika kubadilisha maisha ya wananchi hivyo, ni mategemeo ya jamii kwamba ukusanyaji wa maoni hayo itakuwa chachu ya kuzingatia maslahi ya wananchi pamoja na kuondosha tatizo la uvamizi wa rasilimali hiyo.