NA KIJA ELIAS, KILIMANJARO.
Usawa wa Kijinsia ni moja ya malengo ya Meendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Ukosefu wa usawa wa kijinsia unapimwa kila mwaka na ripoti za Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa.
Usawa wa kijinsia una faida kubwa kwa uhusiano wa kibinafsi wa wanaume, Wanaume wanaoshiriki utunzaji na kutumia wakati mwingi na familia zao wanafuraha zaidi, na wana watoto wenye furaha zaidi.
Kwa kiwango kikubwa, kubadilisha usawa wa mamlaka ni muhimu, sio tu kama suala la haki za binadamu, maendeleo ya kibinafsi, afya na ustawi.
Inaelezwa kuwa uongozi shirikishi ni ule ambao unahakikisha unakuwepo kwa viongozi wanawake, wanaume na vijana ili masuala yote muhimu ya kijamiii ambayo yanarudishwa nyuma yanaweza kutatuliwa.
Mratibu wa mafunzo kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Monica John, anayasema hayo wakati wa warsha ya mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari 35 kutoka mkoa wa Kilimanjaro.
Monica anasema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari, kuangalia uandishi wa habari wenye mlengo wa kijinsia mafunzo ambayo yamejikita zaidi nafasi ya mwanamke katika uongozi.
“Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake ni wachache katika ngazi za maamuzi hata katika uhalisia kutoka katika ngazi ya kata, vijiji na vitongoji hadi kufika ngazi za juu, bado wanawake ni wachache ukilinganisha na wanaume,” anasema.
Anasema “Kama meza ya maamuzi ina jinsi moja yaani wanaume ndiyo wanafanya maamuzi, yale masuala yote yanayowagusa wanawake hayataweza kupewa kipaumbele,”anasema Monica.
Aidha Monica anatoa wito kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuondoa mila na desturi ambazo ni kandamizi zilizopo katika jamii zisizompa fursa mwanamke kushirikishwa katika uongozi ili kuwawezesha kutambua haki zao.
“Mafunzo haya tumeyaratibu katika mikoa minane, lakini yanafanyika katika mikoa mitano, ukiwemo mkoa wa Mbeya, Kilimanjaro, Shinyanga, Morogoro na Rukwa,” alisema.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Kilimanjaro (MECKI) Bahati Nyakiraria, anasema mafunzo hayo yanayotolewa na TGNP yamelenga kutoa fursa kwa wanawake kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Waandishi wa habari kupitia vyombo vyetu vya habari tunayo fursa ya kuhakikisha tunaisaidia jamii kuondokana na mila kandamizi zenye mlengo wa mfumo dume,” anasema Nyakiraria.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo mwandishi wa habari Lucy Ollomi, anabainisha kwamba wanawake wamefanya mengi, sawa na wanaume hususani katika kila nyanja mbalimbali hapa nchini.
Naye Sia Lyimo, anasema kuwa usawa katika nafasi za uongozi wa kutaka kuwa na asilimia 50/50 kati ya wanawake na wanaume ni lazima utimie, kwa wanawake kuanza kujitokeza kwa wingi, kuwania nafasi mbali mbali za uongozi zikiwemo za Urais, Ubunge na Udiwani.
Kwa upande wake Fina Lyimo, anasema ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali za uongozi umeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni, wanawake kwenye Serikali wameleta maendeleo makubwa ya kijamii na mabadiliko halisi katika maisha ya watu.
Fina Lyimo, ameongeza kusema kuwa wanawake wana uwezekano mkubwa wa kutetea uwekezaji katika elimu na afya; na kuleta muafaka katika vyama na masuala ya kawaida.
Mwandishi Hecton Chuwa, anasema kuwa kumekuwa na mfumo wa kiutamaduni ambao umekuwa ukiwafanya wanawake wajione kuwa ni watu wasioweza kufanya lolote bila uwepo wa wanaume na inapofikia wamepata elimu na kazi, jamii huwa inamchukulia kama mtu mwenye dharau asiyeweza kudhibitiwa hivyo kuongeza kundi kubwa la wanawake wasomi ambao hawajaolewa.
Grace Munuo, anawataka wanawake kutoa ushirikiano wanapokutana na waandishi wa habari badala ya kuogopa kuzungumza mtazamo au changamoto zinazowakabili ili kutokomeza ukatili na ubaguzi dhidi ya wanawake, vijana na wasichana ili kuhakikisha wanapata fursa sawa katika umiliki wa rasilimali na nyanja zote za kimaisha.
“Taarifa kuhusu mwanamke zimekuwa zikitolewa kwa kasi ndogo, unakuta msomaji wa taarifa ya habari ni mwanaume, taarifa zenyewe asilimia 90 zinahusu wanaume jambo ambalo tunadhani linapaswa kuwekwa katika usawa kwani nafasi kwa mwanamke inapokuwa kubwa inafanya hata malengo yale ya SDGs yaende kama yalivyokusudiwa,” anasema Munuo.
BAADHI ya wanahabari waliohudhuria katika warsha ya kuwajengea uwezo wana habari namna ya kuandika habari zinazohusiana na usawa wa kijinsia.
Jabir Johnson anasema kikwazo kikuu ambacho kimewekwa bayana katika utoaji wa taarifa hizo ni wamiliki ambao wamejikita katika kuangalia maslahi yao binafsi bila kujali jinsia hali ambayo imekuwa ikiminya taarifa nyingi zitakazompa changamoto mwanamke katika kuijenga jamii.
“Tumegundua kuwa makosa mengine yamekuwa yakisababishwa na waandishi wenyewe, hali ambayo inazidisha uminyaji wa taarifa za wanawake, kwa mafunzo haya nina imani tutakuwa mabalozi wazuri wenye kuibua changamoto za mwanamke,” anasema Johnson.
Mwandishi Patrick Chambo, anasema wakati mwingine Wahariri kwa maoni yao, wamekuwa wakiangalia soko kutokana na namna ya uendeshaji wa chombo husika.
“Wamiliki wakiishi vizuri na wafanyakazi wao itasaidia kupata muda wa kushauriana kwani kuna mawazo mazuri wanayo wafanyakazi wake kuhusu changamoto mbalimbali za wanawake hali ambayo itabadilisha mtazamo wa kuegemea soko zaidi na kuiacha jamii peke yake,” anasema Chambo.
ITIFAKI YA SADC
SADC ambayo ni jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, ambapo mkataba wake wa kikanda uliotiwa saini mwaka 2008 wenye vifungu unaeleza kuondoa utafauti na kuwatenga wanawake katika Nyanja mbalimbali za maendeleo na kuwasaidia katika usawa wa kijinsia nchi wanachama.
Ambapo katika kifungu cha nambari 12 kinasisitiza ushiriki sawa wanawake kufikia asilimia 50/50 kwenye Nyanja za maamuzi, serikalini na taasisi binafsi.
JUKWAA LA UTENDAJI KAZI LA BEIJING
Mpango wa utekelezaji wa Beijing katika maelezo ya dhamira nambari 7 ya mpango huo imeeleza kuhusu uwezeshaji wa wanawake na ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuangalia uwiano wa kijinsia kwenye ngazi zote za uongozi.
ITIFAKI YA MAPUTO
Haya ni makubaliano yaliyofanyika tarehe 11, Julai 2003 nchini Msumbiji katika mji wa Maputo, katika kipengele nambari 9 chamakubaliano hayo imeonesha haki ya kushiriki wanawake katika siasa sambamba na kushiriki katika mchakato wa vyombo vya kutoia maamuzi.
MKATABA WA CEDAW
Huu ni mkataba wa CEDAW wa kimataifa ambao unapinga aina zote za udhalilishaji, mkataba huu umeasisiwa mwaka 1979, katika mkataba huu kwenye kifungu chake cha 7 kimeeeleza wazi wanawake kushiriki katika siasa na maisha ya kijamii.
Pia umeeleza kuweko kwa usawa baina ya mwanamke na mwanamme katika uchaguzi na mchakato mzima wa upigaji kura sambamba na nafasi za kushika madaraka, kwa mantiki hiyo basi CEDAW ni mkombozi kwa wanawake katika Nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.