KIGALI,RWANDA

RAIS  wa Rwanda Paul Kagame amesema anaithamini kamati ya ushauri ya upatanishi ya Mahakama ambayo ilianzishwa hivi karibuni, akielezea kuwa ndio suluhisho jengine katika sekta ya haki.

Kamati ya mfumo huu mbadala wa utatuzi wa mizozo inaongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Profesa Sam Rugege.

“Tunataka Wanyarwanda kukubali zaidi matumizi ya njia hii ya kusuluhisha mizozo kupitia usuluhishi.Hii itapunguza mrundikano wa kesi pamoja na kesi mpya zilizowasilishwa Mahakamani”,Kagame alisema.

Alisema kuwa, kwa hali yoyote, kuna haja ya kuhakikisha watu wanapata haki kwa njia ya kuaminika.

Jaji Mkuu, Faustin Ntezilyayo, alisema kuwa katika mwaka wa Mahakama 2019/2020, kesi zaidi ya 76,300 zilipitiwa,ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia tano ikilinganishwa na mwaka uliopita lakini Mahakama zinakabiliwa na mrundikano wa kesi 52,950.

Jaji Mkuu alisema, zaidi ya kesi 25,350 zilizowasilishwa katika 2019/20 zilikaa kwa zaidi ya miezi sita ikilinganishwa na 13,000 katika mwaka uliopita.

Kuongezeka kwa mrundikano kunatokana na mripuko wa Covid-19, ambao ulisitisha shughuli za Mahakama.

Kwa nia ya kuharakisha utatuzi wa mizozo, Jaji Mkuu alisema, wahusika walihimizwa kuchagua mkutano wa mapema na upatanishi.

“Imebainika kuwa watu wanaotafuta huduma Mahakamani walianza kuelewa jukumu la kumaliza kesi kwa amani kwa sababu kesi ambazo zilitatuliwa wakati wa mikutano ya kabla ya kesi ziliongezeka hadi asilimia sita mwaka jana kutoka asilimia tatu ya mwaka uliopita, wakati kesi 897 zilishughulikiwa kupitia upatanishi,”alisema.

Kamati imeamriwa kutoa ushauri na kukagua matumizi ya upatanishi katika kesi zilizowasilishwa Mahakamani.