ANKARA,UTURUKI
BAADA ya wiki kadhaa za mivutano mashariki mwa bahari ya Mediterania,Ugiriki na Uturuki zimeashiria kuwa na nia ya kuanza mazungumzo kwa nia ya kuimaliza mivutano hiyo, inayohusu utafiti na uchimbaji wa gesi asilia katika eneo hilo.
Waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Motsotakis alikaribisha hatua ya Uturuki kuziondoa meli zake katika eneo linalozozaniwa, na kuongeza kuwa yuko tayari kwa mazungumzo yaliyokuwa yamekwama baina ya nchi yake na Uturuki.
Mazungumzo ya mwisho kuhusu hazina ya raslimali katika eneo la bahari kati ya nchi hizo jirani na mahasimu, yalifanyika mwaka 2016.
Mvutano ulizidi kushamiri mwezi uliopita, baada ya kupeleka meli ya uchunguzi wa gesi na mafuta katika eneo la bahari ya Mediterania ambalo Ugiriki inadai ni lake.
Waziri mkuu Mitsotakis wa Ugiriki alisema kitendo cha Uturuki kuiondoa meli hiyo ni hatua njema, inayozielekeza nchi hizo kwenye meza ya mazungumzo.