NA ABOUD MAHMOUD

NAIBU Katibu Mkuu Umoja wa Vijana CCM Zanzibar, Mussa Haji Mussa, amewashauri vijana na wananchi wote wa visiwa vya Zanzibar kuwachagua wagombea wa nafasi mbali mbali ikiwemo Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa chama hicho ili waweze kuleta maendeleo zaidi.

Katibu huyo, aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kichama  katika maeneo mbali mbali kuwaombea  ridhaa ya kuwachagua viongozi hao ambao wenye nia ya kuibadilisha Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kufikia uchumi wa buluu.

Ziara hiyo ambayo alianzia katika nyumba za kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ‘soba house’ alisema kupitia ilani ya CCM kifungu cha 195 kwenye ukurasa wa 253 ya mwaka 2020 itaanzisha kituo maalum cha kupokea taarifa zote za dawa za kulevya na kufanyiwa kazi .

“Serikali ya awamu ya nane kwa uwezo wa Mungu ambayo itaongozwa na Dk. Hussein, kwa mujibu wa ilani imehakikisha kuwasaidia vijana wote wakiwemo wale waliokuwa wakitumia dawa za kulevya na kuamua kuacha kwa kuwajengea nyumba, lakini pia itaanzisha kituo maalum cha kupokea taarifa zote za dawa za kulevya na kufanyiwa kazi ili kuliondosha tatizo hilo,”alisema.