NA NASRA MANZI

UMOJA wa Vijana Mkoa wa Kusini Unguja, umefanya dua kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa nchi pamoja na wagombea wa nafasi mbali mbali za chama cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza katika Uwanja wa Ofisi ya CCM Wilaya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Juma Mussa Mkali, aliwataka vijana kuwa wazalendo katika nchi  na kutoshawishika na viongozi ambao wameshakuwa wakihubiri uvunjifu wa amani.

Alisema uzalendo  huo kwa vijana  usiwe unatoka katika moyo, lakini unapatikana  katika nyanja tofauti ikiwemo kuhakikisha kulinda amani iliyopo katika nchi.

Pia akizungumzia suala la uchaguzi alisema ni vyema kufuata taratibu za uchaguzi ifikapo tarehe husika kwani kuna maisha baada ya uchaguzi na wananchi watahitaji kufanya shughuli za kimaendeleo.

Hata hivyo alisema chama kinaendelea kushika hatamu kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar  pamoja na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,hivyo ni vyema kufuata kanuni na katiba za serikali bila ya kuharibu mpangilio uliowekwa.

Aliwashukuru waandaaji kwa kuamua kufanya dua hiyo kwani umoja na mshikamano wa vijana pamoja na viongozi wao wa chama utapelekea kukitetea na kukisimamia chama ipasavyo.

Katibu wa Vijana CCM Wilaya ya Kusini  Mkoa wa Kusini Unguja, Ame Abdalla  Nchicheme, alisema lengo kuu  kukiombea chama cha Mapinduzi kuendelea kushika dola pamoja na kuwaombea wagombea na kuitakia amani nchi.