NA ASIA MWALIM
WANANCHI wa mkoa wa Kusini Unguja wameombwa kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwachagua wagombea wake ili kiendelee kusimamia misingi ya amani, utulivu na maendeleo yaliyopatikana.
Wito huo umetolewa na Makamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Taifa, Thuwaiba Edington Kisasi katika ziara ya kamati ya mikakati ya kampeni za CCM ya nyumba kwa nyumba, katika wilaya ya kusini mkoani humo.
Alisema, maendeleo yaliyopatikana nchini, yametokana na uwepo wa amani na utulivu hivyo alisisitiza haja ya kuendelezwa hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.
Alieleza lengo kuu la ziara hiyo ni kuhamasisha wananchi na wanachama wa chama hicho kujitokeza kupiga kura kwa wingi kwa CCM ili kujiongezea kura katika uchaguzi huo.
“Wazanzibari wana imani na Chama Cha Mapinduzi, hatuna budi kukichagua ili kibaki madarakani na kushinda kwa kishindo uchaguzi ujao,” alisema.
Alifahamisha kuwa baadhi ya watu hawana elimu ya upigaji kura, hivyo wameamua kuwahamasisha na kuwaelekeza ili wasipoteze haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa kusini Unguja, Shemsa Abdallah Ali, aliwapongeza wanawake wa mkoa huo kwa juhudi wanazozichukua katika kuendeleza kampeni za kistaarabu.
Mwenyekiti huyo alisema ziara ya nyumba kwa nyumba na mtu kwa mtu imeweza kuibua changamoto zinazoukabili mkoa huo na kujua jinsi ya kuzitatua changamoto hizo.
Alisema kampeni ya aina hiyo ni halisi na yenye kuwapa hamasa ambayo kigezo chake ni kuashiria ushindi wa CCM kutokana na matumaini waliyonayo wananchi wa wilaya hiyo kwa wagombea walioteuliwa na chama hicho.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Tunu Juma Kondo, alisema waliamua kuandaa ziara hiyo ili kuhamasisha zaidi wanawake kujitokeza mapema siku ya kupiga kura.
Alieleza, wanawake wana ushawishi mkubwa katika jamii, hivyo waitumie nafasi hiyo kushawishi makundi mengine kujitokeza na kukipigia kura chama hicho.
“Kuna baadhi ya vyama vya siasa hupita na kuwarubuni wana CCM, kuwatisha na kuwapa maneno ya uongo, lakini sisi tunapita kuwapa moyo na kuwahakikishia ulinzi na usalama wao,” alisema Tunu.
Hata hivyo aliwataka wananchi wa vyama vya upinzani kukipigia kura chama cha CCM ambacho kina sera zinazotekelezeka sambamba na kuwaomba waliotimiza vigezo vya kupiga kura kutoipoteza nafasi hiyo kwani kupiga kura ni haki ya kila mwananchi.
Katika ziara hiyo iliyohusisha pia viongozi wa UWT wa ngazi mbali mbali mkoa na wilaya ya Kusini unguja ilifanyika katika vijiji vya Jambiani, Paje, Bwejuu na Michamvi ambapo viongozi hao mbali ya kuomba kura, walipatiwa elimu ya kupiga kura kwa usahihi.