Dk. Shein awatoa kiukumbi wagombea

Amnadi muwania urais, ampa vitendea kazi

Dk. Mwinyi aahidi kuinua uchumi, huduma za jamii

KHAMISUU ABDALLAH NA MWINYINVUA NZUKWI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, Dk. Hussein Mwinyi ana sifa zote kuwa kiongozi.

Dk. Shein alieleza hayo jana katika uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliohudhuriwa pia na mgombea mwenza wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Alisema, Dk. Mwinyi ana uwezo mkubwa katika uongozi na si mwanagenzi wa siasa kwani ameshawahi kuwa mbunge kwa kipindi kirefu ikiwemo jimbo la Mkuranga na jimbo la Kwahani hivyo ni mtu aliyebobea kisiasa na kitaaluma.

Dk. Shein ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema Dk. Mwinyi ana upeo mkubwa na heshima kwa wakubwa na wadogo na kujiheshimu mwenyewe.

Aliwaomba wananchi wa Zanzibar kutofanya makosa kwa kuwapa uongozi watu wasiokuwa na uwezo, tamaa na badala yake kumchagua Dk. Mwinyi na mgombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wengine wa CCM ili kuendelea kuijenga kimaendeleo Zanzibar.

Aliongeza kuwa Dk. Mwinyi, Dk. Magufuli na mgombea mwenza wake Samia Suluhu Hassan watashirikiana kuuendeleza muungano na mapinduzi ya mwaka 1964 na kuuendeleza ustawi wa jamii ya watu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, akihutubia katika mkutano huo, Dk. Mwinyi alieleza kuwa serikali atakayoiongoza itaendeleza kazi za maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Dk. Mwinyi alimshukuru Dk. Shein kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa 2015/2020 ambayo inatoa sababu ya chama hicho kuomba kura kwa wananchi wa Zanzibar kuendelea kukiamini chama hicho.

Aliyataja maeneo yaliyotekelezwa kuwa ni ukuaji wa wa pato la taifa kwa wastani wa asilimia 6.8, kuongeza pato la mwananchi kutoka shilingi 1,660,000 mwaka 2015 na kufikia shilingi 2, 549,000 kwa mwaka 2019, kukua kwa uchumi umekuwa kutoka tirioni 2.4 mwaka 2015 hadi tirioni 3.1 mwaka 2019.

Alisema serikali ya awamu ya saba imedhibiti kasi ya mfumuko wa bei kutoka asilimia 5.7 mwaka 2015 hadi asilimia 2.7 mwaka 2019.

Maeneo mengine alisema ni usambaji wa umeme kutoka asilimia 70 mwaka 2015 hadi asilimia 90 mwaka 2019, utoaji wa elimu bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari na  kuongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 60 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 72.

Hata hivyo alisema kwa upande wa mjini alisema idadi ya upatikanaji wa huduma hiyo imeongezeka kufikia 80 mwaka 2015 had kufikia asilimia 87 mwaka 2020 sambamba na kutoa huduma ya matibabu bure na kuongeza bajeti ya dawa kutoka silingi milioni 500 hadi bilioni 12.7 mwaka 2020.

Alisema mbali na huduma hizo pia serikali imeweza kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka watalii 1,3300 kutoka mwaka 2015 hadi watalii 53800 mwaka 2019 kujenga kilomita za barabara 129, ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndenge taminal 111, ununuzi wa meli na kuweka taa za bararani kwa Unguja na Pemba.

Akieleza mambo atakayoyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano Dk. Mwinyi alisema ni pamoja na kuzienzi tunu za Tanzania ambazo ni Mapinduzi ya 1964 na Muungano wa Tanzania.

“Tutaendeleza ukuaji wa kasi ya uchumi kwa kutumia uchumi wa bahari lakini pia kujuza utalii kwa kuongeza aina za utalii ambazo zitafungua fursa kwa wananchi wote kwa ujumla,” alieleza Dk. Mwinyi.

Aliongeza kuwa sekta ya uvuvi itaimarishwa ili kuwawezesha wavuvi kuvua katika bahari kuu, kuvua katika maji madogo, ufugaji wa samaki lakini pia kuitumia bahari kuimarisha uchumi wa mafuta na gesi.

Alisema ili sekta hiyo inufaishe nchi kuna haja ya kuweka sheria madhubuti zitakazowafanya wananchi kushiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi badala ya kuwa watazamaji.

Aidha Dk. Mwinyi alielezaneneo jengine la kipaumbele kuwa ni ujenzi wa kilomita 198 za barabara Unguja na Pemba sambamba na kuongeza udahili katika elimu ya juu.

“Eneo jengine katika kuimarisha huduma za jamii, sekta ya afya itaimarikhwa ili kuwa na watu wenye afya bora watakaozalisha mali na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akizungumza tatizo la ajira alisema ilani imeekeza kuongeza ajira 300,000 katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa kuanzisha viwanda Unguja na Pemba.

Kuhusu amani na utulivu alisema iwapo atachaguliwa, ataweka mkazo mkubwa ili amani iendelee kuchochea maendeleo ya nchi sambamba na umoja na mshikamano.

Uwajibikaji, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma Dk. Mwinyi alisema hatokuwa na muhali sambamba na kuwashughulikia wale wote ambao hawaendani na matarajio ya serikali yake katika kukuza uchumi.

Kwa upande wa maovu katika jamii mgombea huyo alisema ataendeleza vita dhidi ya dawa za kulevya, udhalilishaji, dhulma na uonevu kwa kuweka mfumo wa kuwafikia wananchi wa ngazi ya chini.

Akieleza maudhui yaliyomo katika ilani ya uchaguzi wa CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdullah Juma Sadalla alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali itakayoongozwa na CCM itazingatia ustawi wa jamii, amani na ulinzi wa nchi na watu wake.

Mabodi alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Tanzania Dk. John Pombe Magufuli na Makamu wake Dk. Ali Mohamed Shein kwa kusimamia vyema ilani ya CCM ambayo inawafanya kutembelea kifua mbele.

Hata hivyo, alisema wapo watu ambao tayari wameanza kutishia uvunjifu waamani, lakini CCM itaendelea kuhubiri amani na utulivu haitakuwa tayari kumuona mtu anaendelea kuivunja amani ya nchi iliyopo

Katika mkutano huo Dk. Ali Mohamed Shein aliwatambulisha wagombea wa nafasi ya ubunge, uwakilishi na udiwani ambao pia walipata nafasi ya kuomba kura kwa wananchi na kuwakabidhi ilani ya CCM yam waka 2020/2025.