NA ZUHURA JUMA, PEMBA
TIMU ya ATM ya Bomani na Mchezani FC zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muendelezo wa mashindano la Dande cup.
Mtanange huo ulitimua vumbi katika Uwanja Utaani Wete majira ya saa 10:00 jioni.
Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko hakuna timu iliyofunga bao.Kipindi cha pili dakika ya 40 Abdul Mbashir (kibabu) kutoka timu ya ATM alifunga bao, ambapo timu ya Mchenzani ilisawazisha bao hilo mnamo dakika ya 90 kupitia mchezaji Yussuf Ali.
Mchezo mwengine timu ya Al-chicos FC ya Utaani imepokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa timu ya Cossovo FC.Mbarouk Haji wa timu ya Cossovo FC alifunga bao la kwanza katika dakika ya 23 ambalo lilidumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.
Kurudi uwanjani kipindi cha pili timu ya Cossovo FC ilifunga tena bao la pili kwa mfungaji wake Juma Mohamed mnamo dakika ya 53, ambapo timu ya Al-chicos ilipata bao la kufutia machozi kwenye dakika ya 72 kupitia mchezaji wake Abdalla Ramadhan.
Katika uwanja wa Utaani Wete ambapo timu ya Al-kumas ya Bopwe na timu ya TK FC ya Kilorodi ilitoka sare kwa kufungana bao 1-1.
Bao la kwanza lilitiwa wavuni na mchezaji Mahad Juma kutoka timu ya TK FC mnamo dakika ya 19.Baada ya mapumziko timu ya Al-kumas ilisawazisha bao lake mnamo dakika ya 47 kupitia Hamoud Abrahman.