NA ASIA MWALIM

ZAIDI ya vijana 60 wa maeneo tofauti ya visiwa vya Unguja ikiwemo Nungwi wamepatiwa mafunzo ya udhalilishaji wa kijinsia ili waweze kujikinga athari za vitendo hivyo.

Mratibu wa Wanawake Taasisi ya Interfaith Centre, ambae pia ni Mchungaji wa Kanisa la KKT, Rebecca Muhoza, alisema hayo alipokua akifungua mafunzo hayo huko Nungwi Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Alisema endapo vijana na watoto wataendelea kupatiwa mafunzo yanayohusu vitendo vya udhalishaji wa kijinsia na njia sahihi za kuweza kujikinga, kwa kiasi kubwa kutasaidia kupunguza na hata kutokomeza vitendo hivyo.

Aidha alisema vitendo hivyo vimekua vikiendelea kufanyika kwenye maeneo tofauti kwa watoto wa kiume na wakike, jambo ambalo linapelekea kuharibu mustakabali wa maisha yao.

Alifahamisha kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanaondoa vitendo hivyo ambavyo ni changamoto inayo ikabili jamii ya watanzania Sambamba na Kuzima ndoto za watoto hao.

Alisema kuwa licha ya jitihada za Serekali na baadhi ya taasisi kuendelea kutoa elimu hiyo mjini na vijijini, kuna baadhi ya wazazi hawapo tayari kupinga vitendo hivyo jambo ambalo linarudisha mendeleo ya jamii.