NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Hussein Ali Mwinyi awasisitiza vijana kutokubali kuyumbishwa na kutumiwa na watu kwa kisingizio cha kisiasa au dini.

Kauli hiyo aliitoa katika kongamano la siku ya amani duniani lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni. 

Alisema mara nyingi uvunjifu wa amani hauletwi na wazee wala watoto, bali chanzo chake ni vijana kutokana na kukubali kutumiwa na watu ambao hawana nia njema na nchi yao.

Alisema, watu wengi hudhani amani inaletwa na vyombo vya ulinzi na usalama pekee, jambo ambalo sio kweli bali msingi wa amani unaanzia kwa wananchi wenyewe kukwepa kila viashiri vya vurugu.

“Sio idadi ya askari tulionao, ubora wa zana za kijeshi tulizonazo zinazoweza kuleta amani, bali amani huletwa na utulivu wa wananchi na Tanzania tunajivunia kuwa na wananchi wapenda amani,” alisema.

Dk. Mwinyi ambae pia ni mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi alibainisha kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba amani tuliyonayo inaendelea kudumu.

Alifahamisha kuwa zipo nchi ambazo zimeichezea amani katika nchi zao na kupelekea machafuko ikiwemo Syria, Yemen, Iraq, Congo na kwamba yanatoyokea katika nchi hizo iwe fundisho.

Hivyo, alisisitiza kuwa wananchi wana kila sababu ya kudumisha amani iliyopo na kuwa mabalozi wa amani katika nchi yao ili kuendelea kupata maendeleo.

Sambamba na hayo alisema vijana ndio wadau wakubwa wa amani, hivyo ni lazima kutumia nafasi hiyo katika kulaani vitendo vya uvunjifu wa amani popote pale inapotokea.

Alitumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya saba kwa hatua ya kuanzishwa kwa Baraza la vijana Zanzibar ambalo linajenga taifa la baadae litakalotetea nchi yao. 

Hivyo, aliwasisitiza viongozi wa baraza hilo kuendelea kujenga umoja ili kutoa fursa kwa serikali katika kuwasaidia vijana katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Khamis Faraj Abdalla, alisema siku hiyo ina lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa sambamba na kuwapa elimu ya uzalendo katika kulinda amani ya nchi wakati wote.

Nao vijana kutoka vyuo vikuu na mabaraza ya vijana Zanzibar, walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika kusimamia suala la amani ya nchi na kuahidi kuilinda na kuitetea wakati wote ili iendelee kudumu.

Katika kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo wajibu wa jamii katika kulinda amani ya nchi, umuhimu wa kutoa taarifa za uvunjifu wa amani ambapo kauli mbiu ni “Tudumishe amani kwa pamoja”.