NA ASYA HASSAN
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud amewataka Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo kutowaunga mkono wanasiasa wenye lengo la kuwabagua na kuwagawa wananchi kwa maslahi yao binafsi.
Alisema wanaCCM wanaweza kufanya hivyo kwa kujiepusha na propaganda wanazopelekewa kwa lengo la kuwagombanisha na viongozi wao jambo ambalo litapelekea kukosekana kwa vijana wazalendo na wenye maslahi mapana ya taifa.
Mkuu huyo ambae ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa humo, alisema hayo alipokuwa katika zoezi la kuzindua klabu ya ushindi ya Chama Cha Mapinduzi ya Dk. Hussein Mwinyi hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Kibeshi, Unguja Ukuu wilaya ya Kati, Unguja.
“Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakipandikiza maneno yasiyo na tija ndani ya chama na taifa, hivyo kaeni nao mbali kwani CCM imepata mafanikio makubwa ya kuweka umoja, mshikamano, kutokubaguwana na kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema Ayoub.
Aidha alipongeza hatua ya vijana hao na kuitaja kuwa ni ishara ya ushindi wa kishindo wa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika oktoba 28 mwaka huu.
Akizungumzia suala la kuwawezesha vijana, Mkuu huyo wa mkoa alisema serikali ya mkoa huo itahakikisha vijana wake wanawezeshwa kutokana na fursa zilizopo ndani na nje ya mkoa huo.
Akizitaja baadhi ya fursa hizo Ayoub, alisema ni pamoja na utalii, kilimo na biashara hivyo ni vyema vijana kuzitumia fursa hizo ili waweze kujiinua kiuchumi na kujipatia maendeleo.
Sambamba na hayo alitumia fursa hiyo kuwataka vijana kufuata utaratibu na kutumia busara wakati wanapohitaji ufafanuzi wa jambo linalowahusu vijana hao ili waweze kujiepusha na migogoro isiyo na tija kwao.
Kwa upande wa Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) mkoani humo Said Hassan Shaaban, alisema klabu hiyo imeanzishwa kwa lengo la kutafuta kura za wagombea wa ngazi zote wa CCM ili kusudi kuendelea kukibakisha madarakani chama hicho.
“Tunapenda kukuhakishia kuwa katika safari ya kuzitafuta kura kwa wagombea wa ccm, mbali ya ilani ya uchaguzi pia tutazingatia katiba na sheria za nchi,” alifafanua Said.
Akisoma taarifa ya uzinduzi wa klabu hiyo, Katibu wa UVCCM mkoa wa Kusini Unguja, Aboud Said Mpate, aliahidi kuwa chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kitapata ushindi wa asilimiia kubwa mkoani humo katika ngazi zote.
“Tunawaomba wagombea wa CCM kutafuta ushindi kwa mashirikiano pamoja na kuanza matayarisho ya ushindi wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2025, kujenga mashirikiano ya pamoja katika majimbo kwa ngazi ya wabunge, wawakilishi na madiwani,” alisema Mpate ambapo vijana 60 walikabidhiwa kadi za UVCCM.