NA ASIA MWALIM

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limevitaka vikosi vya ulinzi shirikishi mkoani humo kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuilinda na kuitunza amani ilioyopo nchini.

Kamanda wa polisi mkoa huo ACP Awadh Juma Haji, aliyasema hayo wakati wa kikao cha cha vikosi hivyo, huko ofisini kwake Mwembemadema Zanzibar.

Kamanda Awadh alisema vikundi hivo endapo watashirikiana na kuchukua hatua za kuendelea kuilinda amani  hasa kwa wakati huu wa kufunguliwa kampeni sambamba na kuelekea uchaguzi mkuu ambapo wananchini hutegemea amani hiyo.

“Wananchini wa mkoa huu wanahitaji kufanya mambo yao wakiona amani imetawala hivyo hatutasita kuwalinda,” alisema.

Aidha alivitaka vikundi hivyo kufuata sheria na muongozo waliowekewa sambamba na kujiepusha na watu wasioipenda amani na maendeleo ya nchi.

Alifahamisha kuwa lengo la kuanzishwa vikundi hivo na kuwepo askari hao ni kupambana na vitendo vya kihalifu na wahalifu pamoja na vitendo vinavyo vuruga amani ndani ya mkoa huo.

Awadhi alivipongeza vikundi hivyo kwa kujitolea kufanya kazi hizo ambazo lengo lake ni kupambana na wale waliodhamiria kufanya uhalifu pamoja na vitendo vinavyopelekea kuvuruga amani ndani ya mkoa.

Aidha kamanda awadhi alivitaka vikundi hivyo kuacha kutumika kama sehemu ya kufanyia uhalifu kwan kumekuwa na baadhi yao ambao hushiriki kufanya uhalifu kwa kupitia vikundi hivyo.