NA ABOUD MAHMOUD

WANAVIKUNDI vya mazoezi visiwani Zanzibar wameshauriwa kuhamasishana kulinda amani na utulivu katika kuelekea uchaguzi mkuu.

Kauli hiyo imetolewa na kocha Mohammed Omar Said wa kikundi cha Mazoezi cha Islanders Fitness cha Maisara mara baada ya kumaliza mazoezi.

Alisema endapo amani katika nchi itatoweka hakuna kitu chochote kitachofanyika ikiwemo shughuli za maendeleo.

Mohammed alisema wana mazoezi wote wana wajibu wa kusimamia suala la kudumisha amani na utulivu, kwa kuwapa nasaha vijana na wananchi.

Kocha huyo aliwataka wana mazoezi kupuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa, zinazohubiri kuvuruga amani iliyopo.

Alieleza kuwa karibu na uchaguzi mkuu kutakuwa na kauli nyingi kutoka kwa wanasiasa,hivyo ni vyema kwa wanamazoezi na wanamichezo kwa ujumla, kuchagua ipi ina manufaa kwa taifa.

 “Wanamazoezi wenzangu hivi sasa tutasikia kauli nyingi hivyo lazima tuwe makini tuendelee na tunalolifanya kwa ajili ya kulinda afya zetu kikubwa ni kuwaelimisha vijana wenzetu mitaani juu ya umuhimu wa amani,” alisema.