NA HAFSA GOLO

VIONGOZI wa shehia nchini wametakiwa kutatua matatizo yaliyomo ndani ya shehia zao, ili  maendeleo yaimarike na vijana wafate taratibu za nchi.

Wito huo umetolewa na sheha wa shehia ya  Jang’ombe Urusi Yussuf Juma Mtumwa ,  alipokua akizungumza na Zanzibarleo mara baada ya kufungua semina ya uimarishaji ulinzi na usalama iliyofanyika katika shehia hiyo.

Alisema masheha ni miongoni mwa watendaji  muhimu wa serikali hivyo ni vyema kujenga utamaduni wa kuisaidia nchi katika kuhakikisha wanatatua changamoto  na  amani iendelee kudumu ngazi ya shehia.

 “Kumekuwa na baadhi ya viongozi wa shehia hususan masheha wapo nyuma katika kushiriki kuondoa changamoto zilizokuwemo ndani ya shehia zao, ikiwemo kutowaajibisha vijana wanaokiuka maadili na sheria za nchi.

Alifahamisha kuwa jamii imekumbwa na dimbwi kubwa la vijana ambao wamejiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya, na vitendo vyengine vya ukiukwaji wa maadili wakiwa  wanaishi  katika shehia hizo na wengine wakifahamika  lakini hakuna mbinu zinazotumika katika kukabiliana na tatizo hilo.

Aidha alisema, vijana wengine  wameacha kujituma, kujitafutia kipato halali, hivyo hupelekea kuwa tegemezi jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao na shehia kwa ujumla.