NA ABOUD MAHMOUD

KITUO cha ‘Upendo’ kinachotoa  mafunzo ya lugha ya alama, maendeleo kwa vijana na watoto viziwi kimeiomba Serikali kuwasaidia kuwatafutia eneo la ujenzi wa kituo hicho ili kuondokana na usumbufu.

Akizungumza na gazeti hili katika ofisi za kituo hicho Mwanakwerekwe Msaidizi Mkuu wa kituo hicho cha Upendo,Saada Hamad Ali, alisema kutokana na kituo hicho kukuwa kwa kupata vijana wengi wanalazimika kupata eneo lao la kufanyika kazi ambalo litakua maalum kwa kazi hiyo.

Alisema hivi sasa wapo katika nyumba ya kuazimwa ambayo haina dhamana kutokana na wakati wowote mwenyewe akiihitaji itawalazimu kuhama na hawajui watakwenda wapi.

“Naiomba Serikali yetu chini ya kiongozi mkuu Dk Shein kutusaidia kutupatia eneo ambalo litatusaidia kujenga kituo hichi na kitakua katika sehemu maalum ya kudumu,”alisema.

Saada alisema kituo hicho ambacho kilianza na watoto watatu hivi sasa kimeimarika na kupata watoto 43 wanaopata mafunzo hapo ikiwemo kazi za amali.

Alisema wanafunzi wanaojiunga na kituo hicho hutakiwa kusaidia kila mwezi kutoka shilingi 10,000 lakini baadhi ya wazazi wanashindwa kutoa mchango huo na ndio sababi zinazofanya kutoendelea kwa kituo hicho.

“Hapa tunawapa mafunzo watoto mbali mbali wakiwemo wale  ambao hawajaanza kusoma, walioacha skuli na hata wanaotaka kujifunza elimu ya amali, na huwataka wachangine fedha hizo lakini wanafika mwaka hawajatoa na kuwafukuza hatuwezi kwa sababu tumeamua kujitolea lakini kuna vitu muhimu vinahitajika na uwezo wa kununua hatuna,”alisema.