NA KHAMISUU ABDALLAH

ABIRIA na dereva waliopakiana kwenye vespa wakiwa hawakuvaa kofia ngumu huku dereva akikosa leseni ya udereva wametozwa faini ya shilingi 120,000 katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe.

Hakimu Nazrat Suleiman, aliwatia hatiani washitakiwa hao, Richard Abdul Francis (23) mkaazi wa Kilimani ambae ni dereva wa vespa na Abdul Nadhif Shaka Hassan (25) mkaazi wa Kiembesamaki wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ambapo walikubali makosa yao ya usalama barabarani.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Asya alimtaka mshitakiwa Richard kulipa faini ya shilingi 30,000 kwa kosa la kushindwa kuvaa kofia ngumu na kosa la kushindwa kuwa na leseni ya udereva kulipa faini ya shilingi 50000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki mbili kwa kila kosa.

Kwa kosa Abdul mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo kulipa faini ya shilingi 30,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa wiki mbili lakini walilipa faini hiyo, ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo.