NA LAILA KEIS

VYOMBO vya habari vimeelezwa kuwa vina nafasi kubwa ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na salama.

Mkufunzi wa Chuo cha Habari Zanzibar (ZJMMC), Moh’d Mzee, aliyasema hayo wakati akitoa elimu juu ya maadili ya utowaji wa taarifa za uchaguzi, kwa wafanya kazi wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, huko ofisini kwao Maisara mjini Unguja.

Alisema, kufanikiwa kwa uchaguzi, kunategemea vyombo vya habari, kwa kutoa taarifa zilizosahihi na pia kushajihisha amani kwa jamii.

Pia alisema, iwapo vyombo hivyo vitakwenda kinyume, kwa kuchochea machafuko, basi vitapelekea nchi kuingia kwenye vurugu na nchi kukosa amani.

“Vyombo vya habari ni hatari sana, hivyo waandishi wana dhima ya kufata maadili yao, ili uchaguzi upite kwa salama na amani” alisema.

Sambamba na hilo alisema, jamii inategemea zaidi vyombo vya habari katika kupata elimu kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi.

Hivyo watumie vizuri vyombo vyao vya habari, kwa kutoa elimu kwa wapiga kura.

Nae Mwandishi mwandamizi ambae pia ni Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Magazeti, Salim Said Salim, alisema, vyombo vya habari vinatakiwa kutoa habari zenye usawa kwa vyama vyote bila ya kuegemea upande mmoja wa chama.

Pia, aliwataka kutotoa habari zinazotokana na hutuba za chuki au ukabila, ambazo zitapelekea machafuko na sitofahamu kwa wanajamii na aliwataka waandishi kuwa makini Katika kufanya majukumu yao kipindi hichi cha uchaguzi.

“Waandishi lazima muchukue tahadhari ya hali ya juu wakati wa kwenda katika mikutano, msijiache na kujisahau, kwani lolote linaweza kutokea, hivyo muwe tayari kujiokoa” alisema mjumbe huyo.