NA HABIBA ZARALI

KAIMU Meneja redio jamii Mkoani, Saidi Omar Said amewataka waandishi wa habari, watangazaji na watengenezaji wa vipindi kufanya kazi zao bila ya upendeleo hasa katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea uchaguzi mkuu.


Alisema ni wajibu kwa  waandishi wa habari na watangazaji kufuata misingi ya kazi zao, kutenda haki na kutoegemea upande mmoja wakati wa kuandika ama kutangaza habari za kampeni.Aliyasema hayo  wakati akizungumza na wafanyakazi wa redio hiyo kuhusiana na utaratibu mzima wa kuripoti habari za kampeni na uchaguzi mkuu wa 2020.

Alifahamisha kuwa watakapotenda haki kwa vyama vyote vya siasa, wafuasi wa vyama hivyo watakua na imani na waandishi na vyombo vya habari watajijengea heshima na kuepusha malumbano yasiyo na msingi. “Na nyinyi watangazaji muepuke kutumia lugha zisizofaa kwani kunachangia migogoro katika jamii,” alisema.