NA MWAJUMA JUMA TANGA

WAANDISHI wa Habari wa Shirika la Magazeti ya Serikali wachapishaji wa magazeti ya Zanzibar Leo, Zanzibar Mail na Zaspoti, Husna Mohammed Khamis na Zuhura Juma, ni miongoni mwa washindi wa tunzo za umahiri wa uandishi wa habari (EJAT) zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Husna alishika nafasi ya kwanza katika kipengele cha habari za utawala bora na hedhi salama wakati Zuhura alishika nafasi ya kwanza katika kipengele cha habari za jinsia na mshindi wa tatu katika kundi la wazi.

Waandishi wengine wa Zanzibar waliopata tuzo hizo ni Rahma Suleiman (Nipashe) alieshinda katika uandishi wa habari za jinsia na ushindi wa tatu katika uandishi wa habari za utawala bora, Asha Ahmed (Chuchu FM) aliibuka mshindi wa kwanza wa habari za biashara na uchumi wakati Bakari Masoud akishika nafasi ya pili katika habari za usalama barabarani.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela, amesema serikali inaendelea kuimarisha na kutunga sheria kuhakikisha tasnia ya habari inaheshimika.

Aliyaeleza hayo katika hafla ya tuzo za umahiri kwa waandishi wa habari Tanzania (EJAT) iliyofanyika mkoani Tanga usiku wa kuamkia jana.

Alisema vyombo vya habari ni muhimu katika mazingira ya kila siku kutokana na namna ambavyo hutoa habari kwa umma.

Aliwaomba viongozi wenzake wa serikali kuvitumia vyombo vya habari ili kutangaza yale wanayoyafanya.

“Mambo yanayofanyika bila ya kutangazwa na vyombo vya habari huwa hayajulikani, hivyo nawaasa wenzangu tuvitumie vyombo vya habari kufanikisha maendeleo ya nchi yetu,”alisema.

Mapema Mkuu jopo la majaji katika tuzo hizo, Pili Mtambalike, alisema wakati wa kupitia kazi za waandishi wa habari walikumbana na changamoto mbalimbali kutokana na kugundua makosa mengi ambayo mengi yao yanajirejea.

Alitaja baadhi ya makosa hayo kuwa ni habari kutokua na historia ya nyuma, kutokua na vyanzo tofauti vya habari, lugha fasaha na uchache wa habari za uchunguzi.

Katika hafla hiyo, washindi wa jumla walikuwa ni Hilda Phoya kutoka kituo cha Mlimani TV na Halili Habibu Leteacwa kutoka Mwananchi ambo walizawadiwa shilingi milioni tatu kila mmoja.