PARIS,UFARANSA

KATIKA muendelezo wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu barani Ulaya, mbunge mmoja wa chama tawala cha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameongoza wabunge wenzake kutoka kwenye ukumbi wa bunge,kulalamikia uwepo wa mwanafunzi aliyevalia hijabu ndani ya taasisi hiyo ya taifa ya kutunga sheria.

Anne-Christine Lang wa chama cha La Republique En March hivi karibuni aliliongoza kundi la wabunge wenzake wenye chuki dhidi ya Uislamu kuondoka katika ukumbi wa bunge la nchi hiyo, kwa kuwa wanalitazama vazi la staha la hijabu kama nembo ya kujidhalilisha.

Akihalalisha kitendo chake hicho cha kibaguzi na chuki, mwanasiasa huyo alituma ujumbe wa video katika mtandao wa kijamii wa Twitter akisema,”Kamwe siwezi kukubali, ndani ya Bunge la Taifa, kitovu cha demokrasia, mtu aje amevalia hijabu.”

Hii ni baada ya Maryam Pougetoux, Msemaji wa Chama cha Kitaifa cha Wanafunzi nchini Ufaransa (UNEF) kuhudhuria kikao cha kamati ya bunge akiwa amevalia vazi la stara la hijabu. 

Ufaransa imepiga marufuku uvaaji wa mavazi au nembo zinazoashiria ufuasi wa dini fulani kwa wabunge na wafanyakazi wa bunge la nchi hiyo ya Ulaya.

Chama cha Kitaifa cha Wanafunzi nchini Ufaransa (UNEF), Melanie Luce kilieleza kusikitishwa kwake na kitendo hicho cha kibaguzi na kubainisha kuwa, inakera kuona maneno ya chuki yanatamkwa ovyo kwa kisingizio cha ufeministi.

Wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na kampeni za kuichafua dini hii tukufu limeongezeka mno nchini Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni, katika hali ambayo nchi hiyo ndiyo yenye Waislamu wengi zaidi barani Ulaya.

Oktoba mwaka jana, Baraza la Seneti la Ufaransa lilipitisha muswada wa sheria inayowapiga marufuku akina mama wanaovaa hijabu kuandamana na watoto wao katika safari za skuli.