LONDON,UINGEREZA

WABUNGE wa Uingereza wameunga mkono muswada wa sheria ambao utakiuka baadhi ya vipengele vya makubaliano yaliyoafikiwa baina ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya, kuhusu mchakato wa Uingereza kuondoka katika umoja huo marufu kama Brexit.

Hatua hiyo ilifikiwa licha ya malalamiko makali kutoka kwa maofisa wa Umoja wa Ulaya, na upinzani kutoka kwa Mawaziri wakuu wa zamani wa Uingereza na pia baadhi ya wanachama maarufu wa chama tawala cha Conservative.

Muswada huo unaohusu sera ya soko la ndani la Uingereza ulipata kura 340 za kuunga mkono, dhidi ya 263 zilizoupinga, na kwa ushindi huo ulipata ridhaa ya kujadiliwa kwa undani mnamo wiki hii na inayofuata.

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alisema muswada huo ni muhimu kuhakikisha usalama dhidi ya alichokiita vitisho vya Umoja wa Ulaya kuliwekea vikwazo vya kiushuru soko la ndani la Uingereza.