CARACAS,VENEZUELA
WACHUNGUZI wa Umoja wa Mataifa wamemuhusisha Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Katika ripoti yake yenye kurasa 411 iliyochapishwa ,Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli kuhusu Venezuela ulisema umepata ushahidi wa uhalifu uliokuwa na lengo la kuwakandamiza wanasiasa wa upinzani, ikiwemo mpango maalumu wa kuwafunga jela, kuwapoteza, kuwatesa, kuwadhalilisha kingono na kuwauwa.
Kulingana na ripoti hiyo,uhalifu huo ulikuwa ukifanywa tangu mwaka 2014.
Ripoti hiyo vile vile inasema demokrasia na sheria hazizingatiwi nchini Venezuela katika miaka ya hivi karibuni, ikisema bunge la nchi hiyo lililokuwa na wabunge wengi wa upinzani lilifungwa,Serikali ikapanua mamlaka yake na majaji wakawa wanakabiliwa na shinikizo kubwa.