NA KIJAKAZI ABDALLA, MAELEZO  

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwalim Abdullah Mzee amewataka wafamasia kufuata maadili ya kazi zao ili kulinda heshima katika kada yao.

Mwalim Abdalla alieleza hayo katika hotuba yake ya siku ya wafamasia duniani iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo.

Alisema wafamasia ni moja kati ya kada muhimu katika sekta ya afya ambayo inahitaji watendaji waaminifu na wenye uadilifu katika kutekeleza kazi zao.

Alisema wafamasia wana mchango mkubwa katika jamii ikiwemo kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa katika kukinga na kutibu maradhi mbalimbali.

Aliweka wazi kuwa wafamasia wana wajibu wa kuhakikisha usalama wa dawa kwa wagonjwa wakati wa usambazaji hadi kumfikia mtumiaji.

Kutokana na umuhimu wa kada ya afya, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu aliwataka wafamasia, madaktari, wauguzi na wataalamu wa kada hiyo kushirikiana ili kulinda afya za wananchi.

Aliwashauri wafamasia kufikiria njia bora ya kuziendeleza dawa za asili ili kupiga hatua za kimaendeleo kama zilivyo nchi nyengine zikiwemo India na China.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafamasia Zanzibar, Mohammed Kheir liwasisitiza wafamasia kuwa kitu kimoja na kuwa waangalifu katika kutekeleza majukumu yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi wenzao.