BIASHARA imehalalishwa katika sheria za Mwenyezi Mungu na hata kwenye sheria za ndani ya nchi, lakini kwa mazingira ya sasa wafanyabishara wamekuwa wakiifanyakazi hiyo kwa kuijengea mazingira ya kuichanganya na uharamu.

Kila uchao wafanyabishara wamekuwa wakibuni mazingira yenye utata yanayozifanya na kuzijenga biashara zao kuingia kwenye uharamu, kwa lengo la kujiongezea kipato na utajiri.

Kwa mfano wapo wanaojitahidi kupambana kwenye suala la ukwepaji kodi halali zilizowekwa na mmalaka za nchi na wamekuwa wakitumia kila ujanja ili kuzuia kupungua kwa utajiri walionao.

Kitu cha ajabu huku wakikimbia kulipa kodi kwenye mamlaka za serikali, wanashindwa hata kutumia sehemu ya fedha zao kutoa zaka ambayo ni faradhi na sadaka wakihofia kufilisika, huu ni mtihani mkubwa.

Kiuhalisia kabisa kazi ya biashara ni halali, lakini inangia kwenye uharamu serikalini na hata kwenye dini pale haki za wengine kwenye biashara hizo zisipotekelezwa.

Yapo mengi yanayofanyika kwenye kazi ya biashara hapa Zanzibar ambayo hayafurahishi na mengine yanahatarisha hata maisha ya watumiaji wa bidhaa ambao ni wananchi wa kawaida.

Kama kuna mchezo wa hatari ambao umekuwa ukifanywa kwa muda mrefu hivi sasa na wafanyabishara wa vyakula hapa Zanzibar, ni suala la kubadilishwa nembo za bidhaa.

Tabia hii imekuwa ikifanyika kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali na inafanywa kwa siri kubwa kwenye maghala yanatotumiwa na wafanyabishara kuhifadhia vyakula hivyo.

Kwa mfano, mfanyabishara anaingiza nchini bidhaa kama mchele, unga wa ngano na kadhalika, hata hivyo mzigo huo unapoingia kwenye maghala huchakachuliwa kwa kuwekwa kwenye vifungashia vipya.

Kwa maana ya kwamba kama unakwenda dukani kununua mchele basmati, matokezeo yake ukiitia chunguni hauna tofauti na mapembe ama mbaya zaidi ya mapembe.

Haya yote yanafanywa na wafanyabishara wetu bila ya hata kujali afya za wananchi, bila ya hata kujali sheria za biashara, kwani kubadilisha nembo ni kosa la kisheria.